Taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu hali ya dawa za kulevya nchini, inazidi kusikitisha na kuhuzunisha sana!
Taarifa hiyo ilisomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, mjini Dodoma, katika
maadhimisho ya kitaifa ya ‘Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani’.
Pinda anasema tatizo la dawa hizo ni janga la kitaifa hivi sasa nchini.
Anasema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika
biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba,
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa
kwa kujihusisha na dawa hizo.
Pia anasema katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi
za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kuharibu taswira ya nchi na
kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu
wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Anasema mwaka huu pekee kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya
katika eneo la kimataifa la Bahari ya Hindi karibu na nchini .
Ni wazi kuwa kauli hiyo ya Pinda inathibitisha dhahiri kuwa Taifa
linakabiliwa na changamoto kubwa ya kudhibiti tatizo la dawa za kulevya.
Kwa jumla, anasema vita bado ni ngumu kutokana na wanaoendesha biashara
ya dawa hizo kuwa na fedha za kutoa rushwa na kuhonga kwa lengo la
kuzuia kukamatwa.
Kutokana na hali hiyo, anasema hivi sasa biashara hiyo inaendelea kusambaa na kwamba, tayari imeshabisha hodi hadi shuleni.
Anasema hivi sasa mikate, maandazi na askrimu zinazouzwa kwenye shule za msingi, zinawekwa dawa za kulevya.
Pinda anasema vitendo hivyo vinafanya vijana wengi wa shule za msingi na
hata sekondari kuwa na tabia za ajabu, ikiwamo kuingia darasani wakiwa
na kiatu kimoja mguuni, mkufu wenye nyembe na kidani chenye nyembe
kifuani.
Mwisho, anatoa wito kwa kusema vita dhidi ya matumizi na biashara haramu
ya dawa za kulevya inahitaji ushirikiano wa hali ya juu kwa Watanzania
wote.
Kwa wito huo, ningependa nami nitumie fursa hii kutoa ushirikiano katika vita hiyo.
Nikianza kwa kusema matumizi na biashara ya dawa za kulevya,
havikubaliki hasa katika jamii yenye maadili mema na inayoheshimu na
kufuata sheria.
Hiyo ni kwa sababu matumizi ya dawa za kulevya, huchangia makosa mengi
kutendwa. Makosa hayo, ni kama vile wizi, uporaji, ukabaji na hata
ujambazi.
Kadhalika, heshima zimekuwa zikivunjwa. Ni rahisi kwa mtumiaji wa dawa
za kulevya kukaa uchi hata mbele ya wanawe au wakwe zake. Sikwambii
uwezekano wa hata kujamiiana na mmoja wao.
Dawa za kulevya pia husababisha mali nyingi kuibwa, ajali nyingi kutokea na watu wengi kupoteza maisha.
Kwa hali hiyo, ni sahihi kabisa dawa za kulevya kuitwa 'mama ya maasi'. Na kwa hiyo, vita dhidi yake ni wajibu.
Wajibu huo unamhusu mtu mmoja mmoja, familia hadi Taifa.
Vita hivyo vimeanza muda mrefu nchini. Mbinu na silaha mbalimbali
zimekuwa zikitumika kujaribu kushinda vita hivyo. Nafasi katika safu hii
haitoshi kuzitaja.
Kwa bahati mbaya Pinda leo anauambia umma wa Watanzania kwamba, vita hiyo imefeli. Vikwazo? Ni hivyo nilivyovigusia hapo juu!
La kusikitisha na kuhuzunisha ni kwamba, mara zote vinapotajwa vikwazo
vinavyokwamisha vita dhidi ya dawa za kulevya, kiini hasa cha tatizo
huwa hakiguswi kabisa!
Kiini hicho si kingine, bali ni unafiki. Unafumbiwa macho katika vita
hiyo. Kwa unafiki huo, asili ya matumizi ya dawa za kulevya haisemwi!
Kwamba, ni unywaji wa pombe.
Ni ukweli usiopingika kuwa lengo la mnywaji wa pombe ni kulewa.
Sasa, kabla ya dawa za kulevya hazijagunduliwa, wanywaji walikuwa wakinywa pombe ya kawaida.
Pombe ya kawaida ilipoonekana inachelewesha lengo la mnywaji,
ikatengenezwa pombe kali; kama gongo, kangara, chipumpu nakadhalika.
Lengo likiwa kumuwezesha mnywaji kulewa haraka.
Hatimaye, kadiri siku zilivyozidi kwenda, wanywaji wakaizoea pia pombe
kali. Ikafikia kipindi pombe kali nayo ikaonekana kufeli kumharakisha
mnywaji kufikia lengo (kulewa).
Kwa hiyo, pombe kali ilipoonekana inachelewesha lengo, ndiyo sasa
zikavumbuliwa dawa za kulevya. Lengo likiwa lilelile. Kuharakisha
kulewa. Huo ndiyo ukweli, ambao watu hawataki kuusema.
Sasa, leo kupigia debe, kuhamasisha na kuchochea unywaji wa pombe huku
unapiga vita matumizi ya dawa za kulevya, kuna tofauti gani na kumpa
mgonjwa wa malaria vidonge vya kumtibu huku unamdunga sindano yenye
vijidudu vya kuambukiza malaria?
Pia unafiki ulioje kuwaambia watu wenye akili zao timamu kwamba, kuna pombe haramu na pombe halali?
Kwamba, iwapo leo askari polisi mathalan atakutana na watu wawili; mmoja
amebeba bia, mwingine kabeba chupa yenye pombe aina ya gongo,
atashughulika na yule tu wa gongo. Lakini mwenye bia atamuacha!
Unabaki unajiuliza. Hivi lengo la mnywaji wa gongo lina tofauti gani na lile la mnywaji wa bia?
Ukweli lazima usemwe. Kwamba, pamoja na manufaa ya kiuchumi yaliyomo
kwenye biashara ya pombe, madhara yake (pombe) ni makubwa sana kwa
jamii. Maadhali kuna ugumu wa kuzuia na kupiga vita unywaji wa pombe,
vita dhidi ya dawa za kulevya kamwe haitafanikiwa.
Haitafanikiwa pia iwapo wenye mamlaka au jamaa wa wenye mamlaka
wataendelea kuwa sehemu ya dawa za kulevya, na pia vyombo vinavyohusika
na mapambano vitakabiliwa na tatizo la rushwa.
Vilevile, haitasaidia iwapo maadili katika jamii yataruhusiwa kuendelea
kumomonyoka, ikiwamo kuruhusu kila kona ya mji kujengwa ama baa au
grosari!
chanzo: nipashe