MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Tabora leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa hoja za kisheria na
kupanga tarehe ya usikilizwaji wa shauri la maombi ya marejeo katika
kesi ya ugaidi inayowakabili wanachama watano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA).
Shauri la
maombi ya marejeo liliwakilishwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala,
akiiomba mahakama kuu ipitie majalada ya kesi mbili dhidi ya wateja
wake zilizofunguliwa mahakama za chini na kuyatolea maamuzi kwamba
zimeshindwa kutimiza wajibu wake.
Wakili
Kibatala alibainisha katika maombi hayo kwamba uamuzi huo wa mahakama za
chini, umeathiri pia haki za waomba rufaa ikiwamo haki ya kupata
dhamana.
Wiki
iliyopita Jaji wa mahakama hiyo, Simon Lukelelwa, aliahirisha
usikilizwaji wa shauri hilo baada ya kutokea ubishani wa kisheria kati
ya Wakili wa Serikali, Juma Masanja na Wakili wa utetezi, Kibatala.
Jaji
Lukelewa alifikia uamzi huo mara baada ya kukubaliana na maombi ya
Wakili Masanja kwamba walichelewa kupata nakala ya maombi
yaliyowasilishwa mahakama kuu na wakili wa utetezi.
Katika maombi
yake wakili wa serikali aliiambia mahakama hiyo kuwa walipokea nyaraka
hizo Julai 19, mwaka huu, hivyo haikuwa rahisi kuweza kuzijibu.
Pia aliomba apewe nakala za mashauri mawili yaliyofunguliwa katika mahakama za Wilaya ya Igunga na ile ya Hakimu Mkazi wa Mkoa.
Jaji
Lukelelwa aliutaka upande wa serikali uwe umejibu hoja hizo kabla ya
jana ili leo aweze kutoa uamuzi na kupanga tarehe ya kuanza usikilizwaji
wa shauri la maombi ya marejeo lililowasilishwa na Wakili Kibatala.
Watuhumiwa
hao watano ni Kaimu Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry
Kileo, Evodius Justian, Oscar Kaijage, Seif Kabuta na Rajab Kihawa.
Wote kwa
pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kudaiwa kumjeruhi Mussa
Tesha kwa kutumia tindikali na kutenda vitendo vya kigaidi chini ya
kifungu cha nne cha sheria.
NA TANZANIA DAIMA