Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo
katika risala ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani aliyoitoa kwa wananchi kupitia
vyombo vya habari.
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
SERIKALI haitovumilia kuona watu wanaohatarisha
maisha na afya za wengine kwa kuwauzia bidhaa zilizopitwa na wakati, mbovu,bei
ya juu na zisizokuwa na vipimo bora hasa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Dk. Shein alisema wakati watu wanatafuta riziki
katika mwezi huu wanapaswa kuzingatia haki na kuhurumiana katika biashara.
Alisema inafahamika kuwa faida kwa
mfanyabiashara ni lazima, ili aweze kujimudu na kuendelea lakini wakati huohuo
akumbuke kufanya biashara bila ya kupitisha hadaa.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein aliviagiza
vyombo husika kuchukua hatua madhubuti kuhusu masuala ya biashara sambamba na
mazao ya kilimo, kama ndizi zinazouzwa sokoni zikiwa changa.
Alitoa wito kwa wananchi wote kuhurumiana kwa
njia mbali mbali hasa katika kutoa sadaka kwa wasiojiweza, mayatima, masikini,
wanafunzi waliopo daghalia, wagonjwa waliopo hospitali na watu wengine wanaotaka
kusaidiwa angalau kwa futari.
Dk. Shein aliwataka wananchi kuzifuata taratibu
zote alizoziagiza Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa ni pamoja na kuondoa sababu
zote za utengano na mifarakano na badala yake waimarishe umoja, mshikamano,
ihsani na kupendana.
Alisema Ramadhani imekuja wakati wa msimu wa
utalii, hivyo ni vyema kuwa na subira na kuwaongoza wageni juu ya taratibu, mila
na kanuni zilizopo nchini katika mwezi huu bila ya bughudha au uvunjaji wa
sheria.
Aliwafahamisha wafanyabiashara wa vyakula,
mahotelini na mikahawani kuwa wanapaswa kuheshimu khulka, mila na utamaduni wa
Zanzibar na kutofanya mambo ya karaha yatakayopelekea kuwakasirisha wanaofunga.
Aliwataka wasiofunga kuwaheshimu wanaofunga na
hatimae kuifanya Ramadhani iwe kivutio cha wageni kwa utamaduni na ustaarabu wa
Zanzibar.
Aliwahakikishia wananchi kuwa Mamlaka ya Maji
Zanzibar (ZAWA) itafanya kila juhudi ili kuhakikisha maji yanapatikana katika
maeneo mbali mbali.
Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kuwa
waangalifu na kutumia vyakula na maji bila ya israfu.
Katika risala hiyo Dk. Shein alimuomba Mwenyezi
Mungu kuijaalia Ramadhani kuwa yenye mafanikio, kuanzia kwa wafanyabiashara,
wakulima, wavuvi, washoni, waendeshaji darsa za dini, vijana, wazee na wananchi
wote kwa jumla.
Chanzo -
ZanziNews