Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, Bibi Harusi ambaye ni mkazi wa Chanika mjini
Handeni, Levina Mmasi (23) amefariki dunia saa moja kabla ya ndoa yake
kufungwa katika Kanisa la Katoliki la Roma Wilaya Handeni Jumamosi na
hivyo kuilazimu kamati ya maandalizi ya harusi kujigeuza na kuwa ya
msiba.
Kifo
hicho kilichotokea Jumamosi mwishoni mwa wiki iliyopita, kimekuwa gumzo
mjini Handeni huku wananchi wakisema kuwa ni tukio ambalo halijawahi
kutokea katika wilaya hiyo.
Msemaji
wa familia ya marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Firmin Mrimasha,
alisema kuwa chanzo cha kifo cha Levina ambaye alijifungua mwanzoni mwa
wiki iliyopita,ilikuwa ni homa aliyoipata ghafla siku ya Alhamisi na
kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na kukutwa na malaria na
kisha kulazwa kwa matibu.
“Huyu
bibi harusi alikuwa ametoka kujifungua, alikuwa na mtoto wa kiume
kutokana na ujauzito wa miezi saba, ndipo ghafla Alhamisi akapata homa
tukampeleka hospitali alikolazwa na baada ya kupata nafuu, aliruhusiwa
Ijumaa.
“Baada
ya kuruhusiwa akaanza maandalizi ya harusi na Jumamosi ambayo ndiyo
siku ya ndoa yake, alijiandaa lakini ilipofika saa 8.05 akafariki dunia
akiwa nyumbani akisubiriwa kwenda kanisani kufunga ndoa ambayo ilikuwa
ifungwe saa 9.00,” alisema Mrimasha.
Alisema,
“Inasikitisha sana ila imeshatokea yaani marehemu amefariki saa moja
kabla ya ndoa yake na baada ya kifo hicho, mtoto wake naye alifariki
muda mfupi baada ya mama yake kufariki dunia,” alisema Mrimasha.
Akizungumzia
mkasa huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi hiyo iliyogharimu Sh7.7
milioni, Abdi Kipacha alisema kuwa kwake ni tukio la kwanza kutokea
tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi kulisahau.
“Nilishazipangia
kazi kamati za maandalizi, lakini ghafla tukapewa taarifa kuwa bibi
harusi amefariki...Hatukuamini, ikabidi niwatangazie wanakamati wenzangu
kuwa hakuna tena shughuli, bibi harusi amefariki,” alisema mwenyekiti
huyo wa kamati na kuongeza:
“Kitu
tulichokuwa tukisubiri ni kuambiwa bibi harusi angefika saa ngapi,
lakini ghafla tukapewa taarifa za kifo, ilikuwa ni vigumu kuamini lakini
ni kweli imetokea na inasikitisha kwani si jambo la kawaida,” alisema
Kipacha.
Kwa
mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu ni kuwa marehemu alikuwa
Mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na kwamba alikuwa katika
kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti yanamkuta alikuwa
hajapokea hata mshahara wake wa awali.
Akizungumzia
hali hiyo, Padri aliyekuwa afungishe ndoa hiyo, Max Sabuni wa kanisa
hilo Katoliki Handeni alisema: “Nimesikitishwa na tukio hili kwa
kuwa halikuwahi kunitokea...Kilichobaki ni wanandugu kuwa watulivu kwa
kuwa Mungu amechukua kiumbe wake kwa muda alioupanga.”
Aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.