Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Thursday, July 18, 2013

BARAZA KUU LA USALAMA LA JADILI USALAMA WA WAANDISHI WA HABARI


Na Mwandishi Maalum

Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, jana jumatano liliendesha majadiliano ya wazi kuhusu usalama wa waandishi wa habari katika maeneo yenye migogoro.
Majadiliano hayo yaliratibiwa na Marekani ambaye ni Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Julai, na kuhudhuriwa na waandishi wanne wa kimataifa ambao walipata fursa ya kuelezea masahibu wanayokumbana nayo wakati wa kitekeleza majukumu yao.
Majadiliano kuhusu suala la usalama wa waandishi wa habari katika maeneo yenye migogoro ni ya kwanza kufanyika ndani ya Baraza hilo, tangu lilipopitisha Azimio namba 17 38 mwaka 2006 lililokuwa likizungumzia suala hilo. Aidha hii pia ni mara ya kwanza kwa waandishi wa kimataifa kuzungumza ndani ya Baraza Kuu la Usalama.
“ Hapa nilipo mimi ni maiti anayetembea , ninatembea pasi kujua nani anaweza kuondoa uhai wangu,wakati wowote naweza kupotea maisha. naweza kuuawa hata na kijana mdogo ilimradi ana silaha”
Kauli hiyo ilikuwa ni ya Bw. Mustafa Haji Abdinur anayeandikisha AFP akitoka Somalia. Na kuongeza kwamba rafiki zake wengi ambao ni waandishi wenziye tayari wameshapotea maisha na kwamba kwa yeyé kuwa hai mpaka sasa ni kama bahati lakini ni suala la wakati tu.
Naye Bi. Cathleen Carrol ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Associated Press na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Kamati ya Kuwalinda Waandishi ( CPJ) pamoja na kuelezea kwa uchungu mkubwa matukio ya mauaji yaliyowakumbua waandishi wenzake katika maeneo mbalimbali duniani anasema, katika shirika lao kuna eneo ambalo limetengwa maalum kwaajili ya kuwaenzi waandishi wote ambao wamepoteza maisha katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, mwandishi Richard Engel wa NBC news, yeyé pamoja na kuelezea mikasa mbalimbali ambayo amekwisha kumbana nayo yakiwamo ya kutekwa wakati akiripoti matukio ya migogoro, yeyé alikwenda mbalia zaidi kwa kuuliza ni nani hasa mwandishi wa habari.
Bw, Engel alieza kwamba ulinzi wa waandishi wa habari hivi sasa unakuwa mgumu sana tofauti na miaka ya nyuma kutokana na kile alichosema kuibuka kwa makundi mengi yanayofanya kazi za waadishi wa habari.
“ Wakati tukijadili hoja hii ya usalama wa waandishi wa habari, pengine pia ni muhimu tukajiuliza hivi ni nani hasa mwandishi wa habari, je mwanaharakati anaye shika video au kamera na kalamu je naye ni mwandishi, au je na yule mwanamgambo mwenye silaha lakini naye ameshika kamera na kupiga picha je naye ni mwandishi” akahoji Bw, Engel
Anasema kwamba ni jambo la kawaida hivi unapokwenda kwenye tukio fulani kukutana na makundi ya watu kila mmoja akiwa ameshika kamera yake akichukua matukio, na katika mazingira kama haya, ni vigumu kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutofautisha nani hasa ni mwadishi aliyesomea na kubobea kwenye fani hiyo na yupi mwanarakati.
Kwa maoni yake anasema pamoja na hamu ya kila mtu kutaka kutaka kukukusanya habari na kuzisambaza kupitia mitandao ya kijamii, ni vime kujiuliza nani anastahili na anapwashwa kupewa ulinzi anapotimiza majukumu yake na kwa vyovyote vile anasema kama ilivyo kwa wanadiplomasia ambao wanakinga vilevile waandishi waliosomea na wenye weledi na taaluma yao wanatakiwa kupewa ulinzi.
Majadiliano hayo yalifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson, na yalikuwa na mvuto wa ina yake hasa kutoka na kauli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wachangiaji.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu alieleza kwamba hujuma dhidi ya waandishi wa habari ni jambo lisilokubalika kwa kile alichosema ni kubinya uhuru wa upatikanaji na utoaji wa habari, lakini pia ni ukiukwaji wa uhuru wa kujieleza. Akalipongeza Baraza kwa kuitisha mjadala huo
Akasema karne iliyopita waandishi wa habari wapatao 600 walipoteza maisha katika matukio mbalimbali na wengine wakiishia magerezani, huku asilimia 90 ya matukio hayo hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa.
Pamoja na wachangiaji wengi kukiri kwamba mazingira ya ufanyaji kazi kwa waandishi wa habari yamezidi kuwa magumu na hatari, walielezea pia kwamba mazingira hatarishi hayapo tu katika maeneo yenye vita bali hata katika nchi wazofanyia kazi. Ambapo takwimu kutoka CPJ zinaonyesha katika kila waandishi watano kati ya sita wanauliwa wakiwa ndani ya nchi zao.
Wengi wa wazungumzaji walieleza kwamba baadhi ya waandishi ama wamekuwa wakitishiwa maisha yao na familia zao au hata kupoteza maisha kwa kuandika na kuchapicha habari zinazofichua vitendo vya rushwa , vitendo vya jinai au kashfa zinazohusu makundi mbalimbali ya jamii na vilevile kuandika habari za uchochezi kati ya kundi moja na jingine..
Wengine wakaenda mbali kwa kusema wakati mwingine waandishi wenyewe wanajiweka katika mazingira ya hatari kwa kukiuka misingi ya kazi zao, kwa kuandika habari zinazopendelea upande mmoja, au kufanya kazi kinyume cha matakwa na matarajio ya yule anayemfanyia kazi.
Wazungumzaji hao wakatoa wito kwa Baraza kuu la Usalama kuangalia namna bora ya kuboresha ulinzi wa waandishi wa habari katika mazingira hatarishi kama vile vita na migogoro na pia wakatoa wito wito kwa waandishi wa habari kuzingatia misingi ya taaluma zao na kuepuka kujingiza katika mitengo isiyo ya lazima.
Suala lingine lililozungumwa kwa kina ni lile la kutofikishwa mbele ya mkono wa sheria watu wanaotuhumiwa kuwahujumu waandishi wa habari.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...