Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Wednesday, July 10, 2013

ALIYEPORA BODABODA AKITUMIA KISU KILINDI AENDA JELA MIAKA 30

img_3512Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Handeni
Mahakama ya wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, leo imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mkazi mmoja wa kijiji cha Kibirashi wilaya ya Kilindi Ramadhani Samselo(20) baada ya kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha aina ya kisu kwa kumshambulia mwendesha bodaboda na kumpora pikipiki yake.
 
Akitoa huku hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Handeni mkoani Tanga Mh. Patrick Maligana, alisema kuwa ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakamani hapo, na hivyo kumtia hatiani mtuhumiwa pasipo shaka kwa kosa aliloshitakiwa nalo.
 
Awali Mwendesha Mashtaka wa Polisi Nzagalila Kikwelele, aliiambia mahakama kuwa, mnamo Januari 29, majira ya saa 2.00 usiku mwaka huu huko Kibirashi, Ramadhani Samselo(20) akijifanya kuwa ni msafiri, na alikodi (bodaboda) pikipiki  ya Bw. Mngoya Kigono ili impeleke nyumbani kwaske.
 
Alisema akiwa amepakiwa na Bw. Mngoya Kigono(21) ambaye pia ndiye mmiliki wa pikipiki hiyo, na walipofika njiani mtuhumiwa Samselo alianza kumshambulia mwendesha bodaboda huyo kwa kisu sehemu ya mbavuni na mikononi na baadaye kuanguka chini na kumpora pikipiki hiyo.
 
Kikwelele amesema pikipiki hiyo yenye namba za usajili T.959 AXN aina ya Sunlg rangi nyekundu yenye thamani ya shilingi 1,400,000 ilikuwa ni mali ya mlalamikaji Bw. Mngoya Kigono.
 
Alisema mara baada ya mtuhumiwa kuondoka eneo la tukio, mlalamikaji alimpigia simu mmoja ya waendesha bodaboda mwenzake na ndipo walitoka kwa wingi kumfuatilia na kumkuta akiwa amelala chini huku akitokwa na damu nyingi ambapo walimchukua kumpeleka hospitalini huku wengine wakimfuatilia mtuhumiwa.
 
Alisema vijana hao walipofika mbele kidogo walimkuta mtuhumiwa akiongeza mafuta lakini alitimua mbio na kuiacha pikipiki hiyo baada ya kubaini kuwa kumbe alikuwa akifuatiliwa kukamatwa na waendesha bodaboda wenzake.
 
Alisema Polisi walianza kumsaka mtuhumiwa huyo ambaye alikimbilia kwenye machimbi ya madini Arusha ambako alitiwa mbaroni na kurudishwa kujibu shitaka lake katika mahakamani hiyo..
 
Akisoma huku hiyo mbele ya umati uliokuwa umefurika mahakamani hapo wakiwemo waendesha bodaboda wa wilaya mbili jirani za Kilindi na Handeni, Hakimu Maligana, alisema kuwa anatoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa wengine wanaowania mali za watu wengine wakati wakitafuta kipato halali.
 
Hakimu: “Chini ya kifungu namba 287(A) cha kanini ya adhabu sura ya 16, ya sheria za Tanzania, nakutia hatiani, je mtuhumiwa una lolote la kusema kwa nini mahakama hii isikupe adhabu kali kwa kosa analoshitakiwa nalo?
 
Mtuhumiwa: “Hakimu mimi naiachia Mahakama yako kuniamulia vile itakavyoona inafaa kwangu”.
 
Hakimu: “Basi unahukumiwa kifugo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa wale wote wenye nia na mawazo ya kufanya ama wanaofanya makosa kama hayo”. Alimaliza hukumu hiyo na kunyanyuka kitini huku sauti kali ya koooooort, ikisikika.
 
Baadae Askari Polisi walimbeba juu juu mtuhumiwa huyo na kumpakia kwenye Defender na kumpeleka Gerezani tayari kwa kuanza maisha mapya ya kifungwa.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...