Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Mbeya Mjini Malanyingi Matukuta
Na Gordon Kalulunga, Mbeya
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mbeya Mjini
kimesema kuwa Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) wilayani humo
kimefikia hatua ya kujichekesha chenyewe kisha kucheka.
Wakizungumza na waandishi wa habari Jijini Mbeya leo, Umoja huo umesema
kuwa hatua hiyo ya Chadema inatokana na kuona dalili zote za kushindwa
katika uchaguzi mdogo wa kata ya Iyela unaotarajiwa kufanyika June
16,2013.
Katibu wa UVCCM wilayani humo Julius Msaka, amesema kuwa, kutokana na
kampeni zinazoendelea katika kata hiyo na baadhi ya wafuasi wa Chadema
na viongozi wao kufanya fujo kwa wafuasi wa CCM bila kufanywa lolote,
sasa wameamua kujichekesha na kucheka wenyewe.
''Kama vijana, hatutavumilia kuona mwanachama yeyote wa CCM akipigwa na
wafuasi wa Chadema kisha akaachwa, tutawalinda wanachama wetu mpaka siku
ya uchaguzi na hata kupita'' amesema Msaka.
Amesema kutokana na viongozi hao kuona dalili za kushindwa, waliamua
kutumia Gazeti la Tanzania kuandika habari kuwa CCM inajifua kijeshi kwa
maagizo ya Mwigulu nchemba hali ambayo siyo ya kweli.
''Sisi kama vijana wa CCM, tunao utaratibu wa kuwa na makambi kila mwaka
mara mbili si kwa ajili ya uchaguzi tu, bali kwa ajili ya kujifunza
ujasiliamali, ukakamavu na itikadi za chama chetu na tunawahakikishia
kuwa tutaendelea kufanya hivyo bila kuvunja sheria za nchi'' alisema
Msaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM wilayani humo Malanyingi Matukuta,
amesema kuwa vijana wa umoja huo ni walinzi wa chama na viongozi wao
hivyo kambi waliloweka katika shule ya Sekondari Ivumwe ni la wazi na
wala si kwa maagizo ya Mwigulu Nchemba.
''Kwanza tunakanusha habari zilizoandikwa na Tanzania Daima kuwa
tumefanya kambi kwa maagizo ya Mwigulu Nchemba na hii ni propaganda ya
Chadema ili wapate kura za huruma katika kata ya Iyela'' anasema
Matukuta.
Alimshutumu Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Mbeya mjini John Mwambigija
kuwa alitoa taarifa majukwaani kuwa kuna vijana 600 wa CCM ambao
wameweka kampbiu eneo la Itende Sec, Igawilo na Igoma, taarifa alizosema
kuwa siyo sahihi.
Alisema eneo walilokuwa wameweka kambi, hata askari Polisi walifika na
kupiga picha wakiwa kwenye mchakamchaka na mazoezi mengine lakini ajabu
wapinzanzani wao kisiasa hasa Chadema wanadai kuwa wanajifunza mafunzo
ya Janjawidi.
''Mafunzo ya Janjawidi ni lazima uwe na mapanga, Bunduki, shoka au visu.
Lakini vyote hivyo hatukuwa navyo na wakawakurupusha Polisi wakaja pale
lakini hawakukuta madai yao yaliyowaambia kuwa eti tumeteka watu''
anasema Matukuta.
Viongozi hao walitoa wito kwa wananchi wa kata ya Iyela kujitokeza kwa
wingi siku ya kupiga kura na kwamba hakuna atakayedhulika na propaganda
za wapinzani wao kuwa mgombea Richard Shangwi si mtanzania na siyo
Mkristo zimekufa baada ya ukweli kujisimamia na kubainika kuwa ni
Mtanzania na ni Mkristo aliyebatizwa kanisa Katoliki mwaka 1963.
Credit: audifacejackson.blogspot.com