Msanii
wa Filam, nchini, Jaqueline Wolper, akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu Tamasha hilo, wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es
Salaam leo.
Meneja
Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo (kushoto) ni Mkurugenzi wa
Sophia Records walio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, Musa Kissoky.
**************************************
Na Mwandishi Wetu
TAMASHA
la Wazi la Filamu Tanzania maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film
Festival’ mwaka huu linatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Sahara
jijini Mwanza.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika jijini Dar es
Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Consolata Adam alisema,
wanaamini litafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mikakati
waliyoiweka.
Consolata
alisema, tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika viwanja hivyo
kuanzia Julai 1-7, mwaka huu huku kukiwa na filamu mbalimbali
zitakazoonyeshwa katika kipindi hicho.
“Tumejipanga
kufanya uhamasishaji wa kutosha ili kuwawezesha wakazi wa Mwanza na
maeneo ya jirani kuweza kuhudhuria tamasha hili. Tunawakaribisha watu
wote wenye mapenzi na filamu zetu za Tanzania kufika na kushuhudia
tamasha hili ambalo mwaka huu limeboreshwa zaidi,” alisema Consolata.
Naye
Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema kwa
ushirikiano na kampuni ya Sophia Records, ambao ndio waandaaji na
waasisi wa tamasha hilo, wanaamini litafana na kufanikiwa zaidi mwaka
huu.
“Tumeona
jinsi wananchi wanavyozipenda filamu za Tanzania maarufu kama‘Bongo
Movies’ na jinsi walivyo na kiu ya kuwaona wasanii wa filamu ana kwa
ana,”alisema.
Edith
alisema waliingia mkataba wa miaka mitatu wa kudhamini tamasha hilo na
kwa sasa wanalipeleka mikoa mingine kama walivyofanya kwa kulipeleka
Mwanza kutoka Tanga lilikofanyika mwaka jana.
“Tunawaahidi
Watanzania wote kwa ujumla, kuwa tamasha hili litakuwa na mvuto wa aina
yake na hatimae kutumika kulitangaza Taifa letu kupitia tasnia hii ya
filamu ambayo kwa sasa inakua kwa kasi kubwa,” alisema Edith na kutaka
kampuni au taasisi nyingine kujitokeza ili kuwa wadhamini wenza.
Naye
Mkurugenzi wa Sophia Records walio waandaaji na waasisi wa tamasha
hilo, Musa Kissoky alitoa shukrani kwa Grand Malt kulidhamini hivyo
kuliboresha kwa kiasi kikubwa.
“Tunawashukuru
sana Grand Malt na wasanii wa Bongo Movie, hususan uongozi wao, kwa
ushirikiana mkubwa wanaotupatia katika kuhakikisha tamasha hili
linafanikiwa.”
Tamasha
hilo litakuwa likianza asubuhi hadi usiku na kutakuwepo na burudaniu
mbalimbali zitakazosindikiza na hakutakuwa na kiingilio, huku akisema
bendi ya Extra Bongo watakuwepo siku ya uzinduzi.
Wasanii
wote maarufu wa filamu wanatarajia kutua Mwanza Juni 29, ambapo siku
hiyo watajumuika na wakazi wa Mwanza ndani ya Club Lips na siku
inayofuata watashiriki katika shughuli za kijamii katika hospitali ya
Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, ambapo watatoa vyandarua zaidi ya 1000.
Akizungumzia
tamasha hilo, mwigizaji Jacqueline Wiolper alisema, wana furaha kubwa
na wanaamini watapata mengi zaidi wakati wote wa tamasha hilo.
Tamasha
hilo linadhaminiwa kwa mwaka wa tatu sasa na kinywaji kisicho na kilevi
cha Grand Malt kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).