Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Saturday, June 8, 2013

TAKUKURU yapokea malalamiko 94


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida,imepokea malalamiko 94 ya kuomba na kupokea rushwa katika kipindi cha mwaka jana (2012). Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Joshua Msuya alisema malalamiko hayo yaliyopokelewa mwaka jana,yameongezeka ikilinganishwa na malalamiko 85 yaliyopokelewa kwa kipindi cha mwaka juzi.
Alisema kati ya malalamiko hayo,ofisi ya mkoa,imepokea malalamiko 69 na malalamiko 25 yalipokelewa na ofisi za wilaya ya Irmba na Manyoni.

Alisema kati ya malalamiko hayo yaliyopokelewa na ofisi ya mkoa,63 yalihusu idara mbalimbali za serikali na sita yalihusu watendaji wa taasisi binafsi.

"Kwa sasa naomba nisitaje idara za serikali na taasisi binafsi zilizolalamikiwa kwa vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kwa mwaka jana,kwa sababu kitendo hicho kinaweza kuchangia kuharibu upelelezi au uchunguzi ambao bado tunaendelea kuufanya juu ya malalamiko hayo",alisema.

Bila kufafanua,Msuya alisema mwaka jana,jumla ya kesi nane zilizokuwa mahakamani,zilitolewa hukumu na 11 bado zinaendelea.

"Tumepokea taarifa nyingi kwa mwaka jana, kitendo kinachoashiria kuwa baadhi ya wananchi wameweza kupta uelewa juu ya masuala ya rushwa na kujua jinsi ya kupigania haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kufichua vitendo vya rushwa",alifafanua Msuya.

Msuya alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi na watendaji wa serikali na vyama vya siasa wasimamie vizuri raslimali za umma na wakemee kwa nguvu zao zote vitendo vya rushwa katika maeneo yao.

"Vyombo vya habari,viwe mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya rushwa.Viongozi wa dini nao kwa nafasi zao,wanalo jukumu la kukemea vitendo vya rushwa na kuwahimiza waumini wao kushirikiana na serikali kutokomeza vitendo vya rushwa",alisema.


VIA/ http://mtanzania.co.tz
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...