![](http://1.bp.blogspot.com/-_bqq8Suj4mk/UbbI9wmnStI/AAAAAAAAA_o/bJjBqvknPmU/s640/balaa.jpg)
BALAA zito! Siku 13 baada ya kifo cha
mwanamuziki wa kizazi kipya, Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwair’, ripoti
ya daktari inayoeleza sababu halisi ya kifo chake bado utata mtupu kwani
haijawekwa wazi, hivyo kuwafanya wengi kuendelea kuamini uvumi.
Kuhusu uvumi, vitu viwili
vinavyotajwa sana ni ama kifo chake kilisababishwa na kuchanganya madawa
ya kulevya pamoja na vilevi vingine, hivyo kutengeneza sumu iliyomuua
au alibeba mzigo wa unga tumboni ambao ulimchachia na kumtanguliza mbele
ya haki.
Huku tukisubiri ripoti hiyo kuwekwa
wazi, Uwazi lipo kwenye wakati mzuri kueleza kinagaubaga jinsi wasanii
wa Kitanzania walivyogeuzwa makuli wa kubeba mizigo ya madawa ya kulevya
tumboni na kusafirisha kwenda nchi mbalimbali.
SOMA ZAIDI HAPO CHINI :
Habari zinaeleza kuwa wasanii
mbalimbali nchini, wameingia kwenye mkumbo wa kusafirisha unga tumboni
kutokana tamaa ya utajiri na wakati mwingine ni baada ya kuona maisha
yao ya kimuziki hayawaendei vizuri.
Kutokana na kuingia kwenye biashara
hiyo, wasanii hao hususan wanamuziki, hutambuliwa zaidi kwa jina maarufu
la punda, kwa tafsiri kwamba wao ni sawa na mnyama huyo ambaye kazi
yake kubwa ni kubeba mizigo ya binadamu.
Hoja kuhusu jina hilo ni kwamba
wanaobeba madawa ya kulevya tumboni, wanajishusha thamani sawa na punda,
kwani binadamu ni wale matajiri wanaowabebesha mizigo hiyo.
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
USHUHUDA WA SUGU
Ukweli wa jinsi matajiri wauza unga
wanavyowatumia wanamuziki wa Kitanzania kama punda, unapewa nguvu na
ushuhuda aliowahi kuutoa Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’.
Mbunge huyo ambaye anapewa heshima
kwamba ni mmoja wa waasisi wa Bongo Fleva, alimweleza mwandishi wetu
kuwa kabla hajawa memba wa jumba hilo la kutunga sheria, aliwahi
kufuatwa na wauza unga kumshawishi awe anabeba mzigo kwenda nao nje ya
nchi.
“Jamaa waliniambia kwa sababu mimi
nasafirisafiri sana, passport (hati ya kusafiria) yangu itakuwa
imeshagongwagongwa sana, kwa hiyo ni rahisi kwenda nchi tofautitofauti
kwa urahisi, kwa hiyo wakataka niwe nabeba unga.
“Kigezo cha pili waliona kwa sababu
mimi ni mwanamuziki, kwa hiyo ni rahisi watu kuamini ziara zangu ni za
kimuziki. Nilikataa, niliwaambia siwezi kufanya biashara hiyo kabisa,”
alisema Sugu.
Mwaka 2011, mbunge huyo aliwahi
kugusia hilo, wakati akitoa hoja kuchangia bajeti ya Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo kuwa serikali ni lazima iwasaidie
wanamuziki wa Kitanzania kwa sababu wanaibiwa sana, hivyo kuwafanya
vijana kuona kimbilio rahisi la kutajirika ni kuuza madawa ya kulevya.
“Mheshimiwa spika, serikali isifanye
ili kijana wa Kitanzania afanikiwe lazima auze unga, madawa ya kulevya,”
alisema Sugu na kueleza mfano huo wa jinsi alivyofuatwa kushawishiwa na
matajiri wa unga ili naye awe punda.
Jack Patrick.
PUNDA HULIPWA DOLA 3000 MPAKA 5000
Kwa mujibu wa mwanamuziki maarufu wa
dansi nchini (jina tunalo), kwa wastani punda hulipwa fedha kulingana na
umaarufu wake, kwa kuangalia kiwango cha mzigo anaobeba, vilevile nchi
anayopeleka.
“Mara nyingi watu wanalipwa dola 3000
(shilingi 4,800,000) mpaka dola 5000 (shilingi 8,000,000). Binafsi
nilishabeba madawa kutoka hapa Tanzania kwenda China, Botswana na Afrika
Kusini, kila nilipofikisha mzigo nililipwa dola 5000,” alisema
mwanamuziki huyo na kuongeza:
“Kuna kipindi nilinogewa, nikawa
sijishughulishi sana na muziki, kila mara nipo safarini nakwenda
kupeleka mzigo, nikirudi nipo vizuri na dola 5000 zangu. Hivi sasa
nimeacha baada ya watu wangu wa karibu kunishauri na kunieleza kwa
mapana hatari inayoweza kunipata.”
MTINDO WA SASA
Utafiti wa siku za hivi karibuni,
umepata jawabu kwamba wauza unga wengi, wanawatumia wanamuziki na
wasanii mbalimbali kusafirisha mizigo kwa sababu kwao ni rahisi
kugongewa visa katika balozi za nchi wanazokusudia kwenda.
“Kule inaweza kuandaliwa shoo ya
uongo na kweli, wewe unasafiri kwamba unakwenda kwenye hiyo shoo lakini
kumbe ni utapeli mtupu. Kule hauendi kama mwanamuziki, isipokuwa ni
punda tu,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza:
“Fikiria mtu unakwenda kwenye shoo
halafu ukumbini wanaingia watu 40, halafu huyo mwandaaji anakulipa fedha
zako vizuri, unalala hoteli nzuri, ukumbi analipa, kodi anatoa. Hii
biashara ya madawa ya kulevya ina siri kubwa.
Khaleed Mohamed ‘TID’.
“Kinachosikitisha kwa wanamuziki
wenzetu ni kwamba hawajitambui. Watu wanakufa jamani, kukubali
kusafirisha madawa tumboni ni sawa kujiweka katikati ya uhai na kifo.
Zile dawa zikipata joto tumboni huponi. Ukijisahau na kunywa kitu cha
moto ni kifo.”
Mtoa habari huyo aliendelea
kubainisha kuwa wanamuziki wa Kitanzania wengi wanakuwa nchini bila kazi
mpaka wanakumbwa na hali ngumu ya uchumi kutokana na kutopata shoo za
kutosha, hivyo kuwawia rahisi kukubali ofa ya kubeba madawa ya kulevya
tumboni kwenda nchi mbalimbali.
“Hivi sasa kuna wimbi kubwa.
Watakwenda hivyo ila baadaye madawa hufeli tu. Naamini itafika wakati
tutashuhudia vifo vingi vya wanamuziki wetu. Mungu akiniweka hai
nitasema, kwani nawajua wanamuziki wengi punda,” alisema.
Aidha, mtoa habari huyo aliwataja
wanamuziki sita nchini ambao aliwataja moja kwa moja kuwa
wanajishughulisha na usafirishaji wa madawa ya kulevya lakini majina yao
tunayahifadhi kwa sasa.
Ambwene Yesayah ‘AY’