MBUNGE wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM), amehoji lini serikali itapitisha Kiswahili kitumike kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu. Aidha, alisema mwaka 2004, Umoja wa Afrika ulipitisha Kiswahili kiwe ni lugha ambayo itatumika katika mikutano na shughuli mbalimbali.
“Je, serikali imejiandaa vipi kupeleka wakalimani wa
kutosha kutoka Tanzania ili waweze kujipatia ajira?” alihoji.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Amos Makala alisema jitihada zinafanywa na taasisi hizo za
kukuza Kiswahili mojawapo kuandika vitabu vingi vya kufundishia na kuongeza
wataalamu.
“Nasema wazo hilo tumelipokea na sisi ndani ya serikali
tunaendelea kulifanyia kazi na hata wakati tunawasilisha bajeti yetu zilitoka
hoja hizo za kuwa Kiswahili kifundishwe madarasani,” alisema.
Aidha, Makala alikiri kupitishwa kwa azimio hilo na
kuongeza kuwa:
“Kama Tanzania tumeona kuwa hii ni fursa muhimu na
tayari moja ya kazi zinazofanywa na Taasisi za kukuza Kiswahili, BAKITA, BAKIZA
ni kuongeza wataalamu zaidi ili waweze kupata ajira hiyo.”
Aliongeza kuwa Tanzania kama Tanzania mjini Addis Ababa
kuna kituo cha kufundishia lugha ya Kiswahili. Awali katika swali la msingi,
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM) alitaka kufahamu kama nchini Tanzania
kuna Sera ya Lugha.
Pia, alihoji kama ipo, je, sera hiyo ya Lugha imeipatia
hadhi gani lugha ya Kiswahili.
Aidha, alitaka kujua kuna mkakati gani mahsusi wa
kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa ya kufundishia kwa viwango vyote vya elimu hapa
nchini.
Akijibu swali hilo, Makala alisema Tanzania hakuna
andiko mahususi au linalosimama pekee kama Sera ya Lugha, bali suala la lugha
limezingatiwa kama Sura maalumu muhimu ndani ya Sera ya Utamaduni ya mwaka
1997.
Alisema katika andiko hilo la sera ya Utamaduni,
Kiswahili kimetambuliwa kuwa siyo tu lugha ya mawasiliano mapana nchini bali pia
ni lugha ya taifa na mojawapo ya lugha rasmi mbili za Taifa.
Aidha, alisema miongoni mwa mikakati mahsusi ya
kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia ni jitihada zinazoendelea
za wataalamu wa Asasi za ukuzaji wa Kiswahili nchini ambazo ni kuboresha sarufi
ya Kiswahili, kutunga Kamusi za Kiswahili za masomo na taaluma
mbalimbali.