
Tanzania imetajwa kuwa nchi pekee Afrika iliyobahatika kutembelewa na marais watatu wa Marekani wakiwa madarakani.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu Majadiliano ya
Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote yanayoanza leo yakihusisha viongozi
wapatao 20 kutoka nchi za Afrika.
Majadiliano hayo pamoja na masuala mengine, yanahusu matumizi ya
teknolojia katika kuhakikisha uzalishaji wenye viwango na ubora.
Sefue alisema ujio huo wa viongozi na ziara za marais hao wa
Marekani, unatokana na jitihada za Rais Jakaya Kikwete kutembelea nchi
hizo na kujenga nazo uhusiano mzuri.
Alihakikishia wananchi kutokuwa na wasiwasi katika kufanya shughuli
zao za uzalishajimali kwa alichoeleza kwamba ulinzi na usalama ni wa
kutosha na Serikali imejiandaa kuhakikisha wageni wanakaa na kuondoka
nchini salama.
Akifafanua kuhusu majadiliano hayo yanayofanyika Dar es Salaam,
alisema viongozi 20 wanatoka Kenya, Uganda, Benin, Algeria, Comoro,
Zambia, Togo, Malawi, Burkina Faso, Botswana, Gabon, Lesotho na Malaysia
watajadili jinsi nchi inavyoweza kutumia teknolojia kuleta maendeleo
ya wananchi kiuchumi na kijamii.
Alisema Tanzania ilijiandaa tangu mwaka jana kwa majadiliano hayo
katika kanda 11 kwa kushirikisha makundi ya vijana, vyombo vya habari,
vyama vya wafanyakazi, afya na makundi mengine kuhusu mbinu za matumizi
ya teknolojia kuleta maendeleo kwa njia ya ushirikiano badala ya kila
nchi kutafuta peke yake.
Tanzania ilijiandaa tangu mwaka juzi kuwa na mbinu mpya ya kutafuta
maendeleo na kupata matokeo ya haraka kwa kutumia teknolojia, kutokana
na wazo la Rais Kikwete aliloliibua kwenye mkutano wa mwaka juzi
uliofanyika Putrajaya, Malaysia.
Tanzania itaongoza majadiliano hayo ya siku nne, ambayo
yatashirikisha vikundi vya ndani na nje ya nchi, kwa lengo la
kuelimishana na kupeana uzoefu namna ya kutumia teknolojia ili kuleta
maendeleo ya haraka.
Balozi Sefue alisema kutokana na ujio wa viongozi na wageni wengi
nchini, nchi itapata faida kwa kutangaza vivutio vya utalii, biashara na
uwekezaji.
Balozi alisema, ziara ya Obama ni ya pili kwa Afrika ya kwanza akiwa aliifanya Ghana mwaka 2009.
Credit: audifacejackson blog



