TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
09/06/2013
MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA
UTANGULIZI;
Kwanza naipongeza Tume ya Jaji
Warioba kwa kazi kubwa waliofanya ya kuratibu maoni na kuja na
mapendekezo ya katiba mpya ambayo hayakushinikizwa na matakwa ya Chama
tawala cha CCM. Tume imeonyesha ujasiri mkubwa na hakika wahafidhina wa
chama hicho watachukia sana.
Mambo mengi yaliyopendekezwa na Chama
Cha Wananchi CUF yameingizwa katika Rasimu ya Katiba. Mambo hayo ni
pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu, kuruhusiwa mgombea
binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura
zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walio ongoza
kwa kura, Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika
kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu, haki za binadamu na mengine
mengi.
Hata hivyo mambo mengi muhimu kama
vile umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali za nchi kutumiwa kwa
manufaa ya wananchi wote, elimu, afya, mazingira ya kukuza uchumi
unaoleta neema kwa wananchi wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za
mitaa hayajaingizwa ndani ya katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba
imeshughulikia mambo ya muungano.
Mambo ya Muungano ni saba: Katiba na
mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo
ya Nje, Usajili wa
Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mwongozo wa Tume kuhusu utoaji wa maoni
ulijikita katika maeneo yafuatayo; Misingi na Maadili ya Kitaifa,
Madaraka ya Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi, Ardhi,
Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala),
Mihimili ya Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Serikali za Mitaa,
Muundo na Mamlaka yake, Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Mambo mengi muhimu
kwa mwananchi wa kawaida ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa,
umilikaji wa ardhi, haki za huduma za afya na elimu, na matumizi ya
maliasili hayajaingizwa katika katiba hii na yanatarajiwa kuingizwa
kwenye katiba ya Tanzania Bara. Rasimu ya katiba kwa wananchi wa
Tanzania Bara haijakamilika mpaka Rasimu ya katiba ya Tanzania Bara
itakapokuwa tayari. Hotuba ya uzinduzi wa katiba ya Jaji Warioba
haikulifafanua suala hili. Hakuna mantiki ya kupigia kura ya maoni
katiba ya jamhuri ya muungano bila kuwa na katiba ya Tanzania Bara kwa
upande wa bara na marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na katiba
ya jamhuri ya muungano kwa upande wa zanzibar. Katiba ya Tanzania Bara
na katiba ya Zanzibar iwe ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kuwepo kwa rasimu ya katiba ya
Tanzania Bara kutasaidi kuondoa kuweka asasi mbili au tatu zinazofanya
kazi moja. Kwa mfano Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, Mdhibiti na
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa
ya serikali ya Muungano ikafanya kazi pia kwa serikali ya Tanzania Bara
ikiwa wananchi wa Tanzania Bara hawana tatizo na utaratibu huo.
MAPENDEKEZO YA JUMLA;
Haya ni mapendekezo ya awali tu,
mapendekezo mengine yataendelea kutolewa kwa kadri ambavyo tutazidi
kuichambua rasimu hii ya katiba. Natoa wito kwa Watanzania wote
kuhakikisha kuwa wanaitafuta rasimu hii bila kuchoka, kuisoma na
kuielewa na kuendelea kutoa mapendekezo yao kwa tume ya mabadiliko ya
katiba iwe ndiyo lengo kuu.
Kwa sababu tume imetangaza kuwa
itachapisha rasimu katika magazeti ya serikali kwa maana ya HABARI LEO
na ZANZIBAR LEO, tunaona kama huku ni kuififisha rasimu isiwafikie
watanzania wengi zaidi.
Kuna haja ya dhati, tume ikaitangaza
rasimu katika magazeti mbalimbali ya kila wiki na ya kila siku ili
kuhakikisha kuwa rasimu imefikiwa na imesomwa na watanzania wengi. Na
nakala zitakazobakia “returns” baada ya mauzo ya magazeti husika tume
izinunue nakala hizo na izisambaze kwa utaratibu maalum mikoani na
vijijini.
Ni ushauri wetu kwa Tume pia kwamba
baada ya kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali kuyumbishwa na wahafidhina
wasiopenda mabadiliko wanaotokana na CCM. Tume iwe na msimamo na
iangalie wananchi wanataka nini na itetee masuala ya msingi na ya
maslahi ya wananchi ambayo inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi ya
taifa na hasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi.
Na mwisho, Tume ihakikishe kuwa
masuala haya tunayoyashauri kwa awamu yanapewa uzito na tafakuri pana
ili kuipata katiba itakayokuza uchumi imara, kuongeza ajira kwa vijana
na kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
“Mungu Ibariki Tanzania”
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Mwenyekiti,
09 Juni 2013, Dar Es Salaam.