KAIMU
Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Dar es
Salaam, Henry Kilewo, anashikiliwa na polisi kwa siku ya tatu leo,
akihusishwa na tukio la kumwagiwa tindikali, Musa Tesha.
Tesha
alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana Septemba 9, mwaka juzi kwenye
kampeni ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, uliomuweka madarakani Dk.
Kafumu Dalali.
Akizungumza
juzi na Tanzania Daima kabla ya kufika makao makuu ya Jeshi la Polisi,
Kilewo alisema hajui anachoitiwa na kwamba anatekeleza wito wa jeshi
hilo kuwa afike ofisini kwao.
“Sijui
ninachoitiwa, nimepigiwa simu naenda kutekeleza wito, nimesha wataarifu
mawakili wangu ninaowaamini, kwa kuwa chochote kinaweza kutokea cha
msingi Watanzania wapenda mageuzi waniombee kwa Mungu,” alisema Kilewo.
Wakili
wa Kilewo, Peter Kibatala, alisema baada ya mteja wake kuhojiwa kwa
muda wa saa tano juzi alielezwa kuwa anapelekwa Igunga, mkoani Tabora
kuunganishwa na watuhumiwa wengine katika kesi ya kutumia tindikali na
kujeruhi.
Kibatala
alisema anasikitishwa na hatua ya jeshi hilo kumnyima dhamana mteja wake
ilhali kosa wanalomtuhumu linadhaminika na kwamba hayo ni matumizi
mabaya ya madaraka kumzuia mtu kwa zaidi ya saa 24 pasipo kumfikisha
mahakamani.
Wengine
wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutumia tindikali na
kudhuru watu ni pamoja na Oscar Kaijage wa Shinyanga na Evodius
Justinian wa Bukoba.
Evodius
Justinian alikamatwa na Jeshi la Polisi mjini Bukoba na kushikiliwa kwa
siku kadhaa kabla ya kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam.
Kabla ya
kusafirishwa na kufikishwa jijini Da r es Salaam, Justinian alieleza
kuteswa na kupigwa na askari waliokuwa wakimzuia katika vituo mbalimbali
kuanzia mjini Bukoba.