HATUA
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza rasimu ya Katiba mpya siku
chache zilizopita, imeibua fukuto jipya la kisiasa lenye mwelekeo wa
kuipinga.
Tayari
baadhi ya wanasiasa kutoka vyama mbalimbali hususan wale wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), wamekwishakaririwa wakieleza kutokubaliana nayo kwa
madai kuwa haiendani na mfumo wa siasa za kileo na kwamba imelenga
kuongeza mzigo wa uendeshaji wa Serikali.
Mbali na wanasiasa mmoja mmoja, waliokwishatoa maoni yao yenye mwelekeo
wa kutokubaliana na baadhi ya vipengele katika rasimu hiyo, CCM
kimetangaza kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC) kwa ajili ya
kuijadili.
Tangazo la kuitishwa kwa CC ya CCM, lilitolewa mjini Dar es Salaam jana
na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana, mbele ya waandishi wa habari
ambaye alieleza kuwa itakutana Jumatatu ya wiki ijayo, kwa ajenda moja
tu ya kupitia kwa undani rasimu ya Katiba mpya.
Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya chama hicho, zimeeleza kuwa mjadala
unatarajiwa kuwa mkali wakati wa kujadili suala la Serikali tatu, ambalo
tangu kutangazwa kwa rasimu hiyo ikipendekeza hivyo, baadhi ya vigogo
waliokwishatangaza au kuonyesha nia ya kuwania urais wamekuwa katika
sintofahamu ya nini cha kufanya.
Ni sintofahamu hiyo, inayoonekana kukikumba pia CCM ambacho kupitia
kwa Kinana kimeeleza kuwa CC itakayoketi Jumatatu, itaangalia kwa undani
iwapo rasimu ya Katiba mpya, itakidhi matakwa halisi ya wakati huu.
“Siwezi kuzungumzia msimamo wa chama kuhusu rasimu hiyo kwa sasa hadi Kamati Kuu ya chama, itakapokuwa imekaa Jumatatu ijayo.
“Si busara kuharakisha kuzungumzia suala hilo kabla chama hakijakaa
na kuichambua kipengele kwa kipengele, kuona kama inakidhi hali halisi
ya matakwa ya kisiasa tuliyo nayo sasa,” alisema Kinana.-Wakati Kinana
akieleza hayo, duru za kisiasa kutoka ndani ya CCM, zinaeleza kuwa
Rasimu ya Katiba mpya imeibua hali na wasiwasi kwa vigogo wa chama hicho
wanaohofia chama chao kupoteza nguvu za mamlaka ya dola kutokana na
upepo wa kisiasa unavyovuma sasa nchini.
Wadadisi na wafuatiliaji wa mambo walio ndani ya CCM, wanaeleza iwapo
muundo wa Serikali tatu za Zanzibar, ya Tanzania Bara na ile ya Jamhuri
ya Muungano kama zilizopendekezwa na Tume ya mabadiliko ya Katiba
utaridhiwa, CCM kinaweza kuambulia ukuu wa Serikali ya Muungano pekee.
Imani hii ya wadadisi na wafuatiliaji wa mambo, inajengwa katika
msingi wa uungwaji mkono na wananchi kwa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kwa upande wa Tanzania Bara na Chama cha Wananchi
(CUF) kwa upande wa Zanzibar.
Kwa msingi huo, haina shaka kuwa CUF ambacho kina nguvu kubwa ya
kisiasa kwa upande wa Zanzibar, kinaweza kuibuka kidedea katika
kinyang’anyiro cha urais, huku Chadema kinachoendelea kujipatia umaarufu
na uungwaji mkono mkubwa wa wananchi kikichukua udhibiti wa Serikali ya
Tanzania Bara na kukiacha CCM kikibaki na udhibiti wa Serikali ya
Muungano ambayo kinaweza kushinda kutokana na historia yake ya kusaka
ushindi wa jumla.-
Wakati wadadisi na wafuatiliaji wa mambo wakitoa tathimini hiyo kwa
upande wa vyama, wachambuzi wa siasa za ndani ya CCM wameeleza kuwa,
iwapo chama hicho kitapoteza nguvu ya udhibiti za Serikali za Tanzania
Bara na ile ya Zanzibar na kubaki na Serikali ya Muungano pekee, hilo
linaweza kuwa anguko lake la kiuchumi.
Inaelezwa CCM kikiwa na udhibiti wa Serikali ya Muungano, hakitakuwa
na ardhi ambayo kimekuwa kikiitegemea zaidi kwa ajili ya kujiendesha
kiuchumi jambo ambalo litakifanya kitegemee zaidi misaada ya wahisani.
Baadhi ya wataalamu wa uchumi, waliozungumza na gazeti hili kwa
sharti la majina yao kuhifadhiwa kuhusiana na mwenendo huo wa mambo,
walieleza kuwa CCM kikiwa na udhibiti wa Serikali ya Muungano,
hakitaweza kujiendesha na pia kitashindwa kuwahudumia wananchi kwa
sababu kitakuwa tegemezi kwa wafadhili kama vilivyo vyama vya upinzani
hivi sasa.Vyama vitavyonufaika na mfumo mpya wa uundwaji wa Serikali
kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu, ni kile ambacho kitakuwa na
udhibiti wa dola ya Zanzibar, ambacho kitadhibiti ardhi, rasilimali na
uchumi wa jumla na kile ambacho kitashika dola Tanzania Bara ambacho pia
kitakuwa na ardhi na kumiliki rasilimali za nchi.
Mambo haya ndiyo yanayoonekana kuwaumiza vichwa wanasiasa na vyama
ambavyo vimekuwa vikipambana kuwania ukuu wa dola, ambapo tangu Juni 3,
siku ambayo Jaji Joseph Warioba, alitangaza rasimu ya Katiba mpya
iliyokuwa ikipendekeza kuwepo kwa muundo wa Serikali tatu, fukuto la
kisiasa kwa wanasiasa walioonyesha tamaa ya urais na vyama vinavyoiwinda
Ikulu, limepanda.Ndani ya CCM, kuna vigogo kadhaa ambao wameonyesha nia
ya kugombea urais mwaka 2015, ambao Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa,
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano), Stephen Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernad Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta.
Kwa upande wa Chadema, watu ambao wanatajwa kuonyesha nia ya kugombea
urais ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa, Naibu Katibu
Mkuu, Kabwe Zitto na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Lakini Chama cha Wananchi (CUF) nacho hakiko nyuma, kwani Mwenyekiti
wake, Profesa Ibrahim Lipumba amekwisha tangaza nia ya kugombea urais
kwa mara ya nne mwaka 2015.
Credit: audifacejackson.blogspot.com