
MKURUGENZI
wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare kuwa nje
kwa dhamana. DPP aliwasilisha kusudio hilo katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu mwishoni mwa wiki, baada ya mahakama hiyo kumwachia
Lwakatare kwa dhamana Juni 11 mwaka huu.
Lwakatare
na Ludovick Joseph walikubaliwa kupata dhamana mbele ya Hakimu Mkazi
Aloyce Katemana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika,
wanaotoka katika taasisi zinazotambulika kisheria ambao kila mmoja wao
atasaini dhamana ya Sh milioni 10 pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hakimu Katemana aliwataka washtakiwa hao kusalimisha hati zao za
kusafiria mahakamani na hawataruhusiwa kuwa nje ya Dar es Salaam bila ya
kuwa na kibali cha mahakama. Ludovick alishindwa kutimiza masharti yuko
rumande.
“Mshtakiwa wa kwanza ametimiza masharti ya dhamana, hivyo atakuwa nje
kwa dhamana hadi Juni 24 mwaka huu na ahakikishe anafika mahakamani kila
kesi inapotajwa.
“Mshtakiwa wa pili utaendelea kuwepo rumande hadi utakapokamilisha
masharti ya dhamana wakati wowote,” hayo yalikuwa maneno ya Hakimu
Katemana siku alipokubali kuwapa dhamana washtakiwa hao.
Lwakatale na Ludovick walikubaliwa dhamana baada kufutiwa mashtaka
matatu ya ugaidi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kubakiwa na
shtaka moja la kula njama ya kumdhuru kwa sumu Dennis Msacky.
Katemana baada ya kupitia hoja za kuomba dhamana zilizotolewa na Wakili
Peter Kibatala alikubali kuwapa dhamana washtakiwa hao, kwa sababu
shtaka linalowakabili lina dhamana kisheria.
habari NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
PICHA - CHINGAONE BLO LIBRARY
chanzo - mtanzania