Mwili
wa dereva wa bodaboda mjini Singida Hamisi Mkimbu, ukiwa barabarani
baada ya kugongwa na basi la Mgamba na kufariki papo hapo. Hamisi
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 28 na 32, aligongwa katika
barabara kuu ya Dodoma – Mwanza eneo la Kuvu Utemini mjini Singida.
Pikipiki
iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Hamisi Mkimbu (bodaboda) baada ya
kugongwa na basi la Mgamba T 759 AVJ lililokuwa linatokea Arusha kwenda
Mwanza. Dereva Hamisi alifariki dunia papo hapo.
Askari kanzu wakiubeba mwili wa dereva wa bodaboda Hamisi baada ya kugongwa na basi la Mgamba.
Mwili
wa dereva wa bodaboda Hamisi ukiwa umelazwa kwenye gari la polisi kwa
ajili ya kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya
mkoa mjini Singida.
Baadhi
ya wananchi wa Singida mjini, wakiangalia mwili wa dereva wa bodaboda
Hamisi (haupo kwenye picha) baada ya kugongwa na basi la Mgamba. (Picha
zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mfanyabiashara
wa kusafirisha abiria kwa pikipiki (Bodaboda) mjini Singida Hamisi
Mkimbu, anayedhaniwa kuwa na umri wa miaka kati ya 28 na 32, amefariki
dunia papo hapo baada ya kugongwa na basi la kampuni ya Mgamba.
Kijana huyo alikumbana na dhahama katika barabara kuu ya Dodoma – Mwanza eneo la ‘kuvu’ kata ya Utermini mjini Singida.
Akizungumzia
ajali hiyo shuhuda Juma Rajabu, amesema wakati Mkimbu (marehemu) akiwa
amefuata barabara hiyo kuu akitokea maeneo ya uwanja wa Namfua
akielekea Bomani, kwa nyuma alikuwa anafuatwa kwa karibu na basi la
Mgamba lenye namba za usajili T 759 AVJ lililokuwa linatokea Arusha
linaelekea jijini Mwanza.
Akizungumza
kwa masikitiko makubwa Rajabu amesem “Mkimbu alipotaka kukata kona
aingie barabara ndogo inayoanzia Kuvu kuelekea kituo cha mafuta cha
Esso, kwa vile basi la Mgamba lilikuwa karibu naye sana,lilimgonga kwa
nyuma na kusababisha kifo chake papo hapo”.
Rajabu
amesema ni kawaida kwa magari makubwa hasa malori aina ya semi na
mabasi, maderava wake wamejenga utamaduni wa kuwadharau waendesha
pikipiki na kuwaona kama vile hawana haki ya kutumia barabara.
Akifafanua
zaidi, amesema kuwa kutokana na dharau zao hizo, madereva hao huwa
hawana tahadhari yo yote pindi wanapoiona pikipiki ipo barabarani.
Amesema
“Hawajishughulishi kabisa kuangalia ‘indiketa’ za pikipiki wala kutoa
nafasi na mwendesha pikipiki aendeshe kwa amani na usalama.
Mwendesha pikipiki atabanwa kwa makusudi hadi ajione kuwa yeye hapaswi kutumia barabara.
Huyu dereva kama angechukua tahadhari kwamba kuna chombo cha moto mbele yake, sitegemei kama tukio hilo lingetokea”.
Mkimbu ambaye inaelekea hakuvaa kofia ngumu, alipasuka kichwa na ubongo ukamwagika barabarani na kuvunja damu nyingi.
Juhudi
za kumpata Kamanda wa jeshi la polisi kuzungumzia ajali hiyo, zimegonga
mwamba baada ya kuelezwa kuwa Kamanda anaendelea na kikao.