Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Sunday, June 9, 2013

ASILIMIA 20 YA BAJETI YA SERIKALI KWA WIZARA ZAKE HUTAFUNWA KWA NJIA YA RUSHWA.

Hon Dr Festus Bulugu Limbu (MP) 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
ASILIMIA 20 ya bajeti ya serikali 'hutafunwa' kwa njia ya rushwa na kukwamisha shughuli za maendeleo nchini kutofikia malengo.

Mbunge wa Magu Mjini (CCM), Dk. Festus Limbu (Pichani), alisema hayo wakati akiwasilisha mada ya majukumu ya kamati za kudumu za Bunge katika mapambano dhidi ya Rushwa nchini na nini kifanyike.
“Inakadiriwa kuwa asilimia 20 ya bajeti ya Serikali huliwa na rushwa kila mwaka,”alisema Dk. Limbu na kuongeza kuwa taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mapendekezo ya Kamati za Bunge hayafanyiwi kazi ipasavyo na serikali.
Semina hiyo ya kuwajengea uwezo wabunge iliyoandaliwa na Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) iliwahusisha wabunge na wanachama wa Chama cha Wabunge walio katika mapambano dhidi ya rushwa (APNAC).
Naye Mkuu wa shule ya Sayansi za jamii Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa David Mwamfupe, akitoa mada kuhusu "Changamoto zinazoliokabili Bunge na serikali katika mapambano ya rushwa nchini na suluhisho lake" alisema mwingiliano wa kisiasa ni miongoni mwa changamoto zinazokabili mapambano hayo.
“Vita hii inatishia nafasi zetu za kisiasa na maslahi binafsi na baada ya kuona tishio lazima mtu ajihami hata kwa kutumia rushwa yenyewe,”alisema.
Wakichangia katika semina hiyo, wabunge walitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Bunge kuwaelimisha wapiga kura juu ya wajibu wa mbunge ili kuondoa vitendo vya kuomba rushwa kwa njia ya kudai huduma ambazo sio wajibu wao.
Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere aliwataka wananchi kutowashinikiza kutoa rushwa kwa kushinikiza kupewa huduma ambazo si wajibu wa wabunge.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keisy alisema kugundua kuwa kiongozi yoyote anapokea rushwa ni rahisi kwa kuwa wanaweza kupiga mahesabu ya idadi ya thamani ya mali zake kama inalingana na mapato yake.
Pia alisema vyombo vya dola viache kuwakamata watumishi wanaotoa ama kupokea rushwa ndogo ndogo kwa sababu hizo ni zawadi tu.
Mbunge wa Manyovu (CCM), Albert Ntabalile, alisema Serikali ni chanzo cha rushwa kwa kuwa huduma zinazotolewa hazikidhi mahitaji ya wananchi.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Moza alitaka Takukuru kujisafisha yenyewe kwasababu huwa havina siri vinavyopewa taarifa za rushwa.
Akijibu Waziri wa Nchi Utawala Bora, George Mkuchika, alisema kuwa maandalizi ya kubadilisha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kuwa Tume ya Maadili ya Viongozi yameshakamilika na mapendekezo yapo serikalini.
Alisema lengo ni kukiongezea nguvu chombo hicho, kiweze kuwa na meno ya kutoa adhabu kwa wale watakaokutana na makosa ya kukiuka maadili.
Aidha, alisema bado suala la Takukuru kuwakamata watu na kupeleka faili kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), kwa ajili ya kutoa kibali cha kushtakiwa limekuwa katika mjadala wa kubadilisha utaratibu huo.
Alisema kutokana na Takukuru kutokuwa na mamlaka ya kumshtaki mtu moja kwa moja ndio maana vyombo hivyo vimekuwa vikilalamikiwa kuwa vinatupiana danadana vinapolizwa kuhusu kesi mbalimbali za rushwa.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...