Chenge ashinikiza mikataba isainiwe bila sera
Chenge
ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi naye alipata nafasi ya
kuchangia katika rasimu hiyo ambapo alisema kuwa wabunge wanaweza
kukataa nchi isichimbe gesi kwa kumsingizia hayati Mwalimu Julius
Nyerere aliyetaka wapatikane wataalamu wetu kwanza. Alisema watu
wamekuwa wakimsingizia Nyerere kuwa alizuia rasilimali zisichimbwe na
kufafanua kuwa wabunge wapende au wasipende lazima nchi iingie kwenye
mikataba hiyo haraka. “Watanzania
tusiogope, sisi ndio viongozi wa sasa. Tuangalie penye kasoro na
tusahihishe. Lakini napenda kuwahakikishia kuwa hatujawahi kufanya mambo
gizani,” alisema.
MBUNGE
wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) amemlipua Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wa zamani, Andrew Chenge, akisema kuwa alishiriki kwenye mikataba ya
madini, lakini hakuitendea haki nchi yake. Halima alitoa madai hayo jana
mjini hapa katika semina kwa wabunge kuhusu rasimu ya sera ya gesi
asili iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini na kufanyika katika
Ukumbi wa Pius Msekwa. Mbali na Mdee pia baadhi ya wabunge nao
walizungumza wazi kuwa viongozi walioishauri nchi kuingia katika
mikataba ya kifisadi ndiyo hao hao wanaisukuma ifanye haraka kuingia
tena kwenye mikataba ya gesi asili hata kabla ya kuwepo kwa sera, sheria
na kanuni.
Mdee
alisema kuwa serikali imepuuza vurugu za kugombea rasilimali hiyo
zilizotokea Mtwara na Lindi, na hivyo akataka umakini uwepo kwenye sera
na sheria mpya ya gesi ili nchi isirudi kwenye mikataba mibovu kama ile
ya madini ya migodi ya Geita, Bulyankhulu na mingine. “Mheshimiwa Chenge
alishiriki kuishauri serikali kwenye mikataba ya madini, lakini
hakuitendea haki nchi yetu,” alisema Mdee.
Hoja
ya Mdee ilikolezwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy (CCM) ambaye
licha ya kutomtaja Chenge kwa jina, lakini alionekana kumlenga yeye
kwani wakati huo ndiye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali. Alisema
wataalamu walioiingiza nchi kwenye mikataba mibovu wakatwe vichwa na
kuitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni ile ya ununuzi wa rada na
ubinafsishaji wa Shirika la Ndege la Taifa (ATC).

Slyvester Mabumba Mbunge wa Dola ampinga Chenge
Kauli
yake ilionekana kupingwa na baadhi ya wabunge ambapo Mbunge wa Dole,
Slyvester Mabumba alipoinuka kuchangia alianza kuomba radhi kuwa
asieleweke vibaya kwa atakachokisema. “Walioiingiza nchi kwenye mikataba
mibovu ya Richmond na IPTL yawezekana wamo humu ndani, hivyo kama
wizara wanakiri kuwa bado hatuna wataalamu wa kutosha tunaharakia nini?”
alisema na kuhoji.
Mbuge (CUF) Magdalena Sakaya amwonya Chenge
Madgalena
Sakaya wa Viti Maaalumu (CUF) alipingana na kauli ya Chenge ya kuitaka
Tanzania ifanye haraka kuingia mikataba ya utafutaji na uchimbaji gesi
asilia akisema kuwa wananchi wameishaumwa na nyoka. Alisema kuwa sera na
sheria ya gesi asilia lazima iseme kuhusu utunzaji wa mazingira kwani
ile ya mafuta ilikuwa kimya na hivyo kuwapa mwanya wawekezaji kuharibu
mazingira watakavyo. “Serikali hii siyo ya kwanza wala ya mwisho, sasa
kutaka kila kitu kifanyiwe kazi leo inaonesha kuwa hakuna nia njema.
Viko vizazi vitakuja na ujuzi mwingine, haraka hii ya nini ya kutaka
kumaliza kila kitu,” alisema.
Ezekiel Wenje (CHADEMA) - Aliyekuibia nyumbani mwako hawezi kuwa mlinzi wa mali yako
Mbunge
wa Nyamagana, Ezekiel Wenje aliunga mkono kauli ya Mdee akisema kuwa
lazima kuwe na uwazi kwenye mikataba ya gesi itakayosainiwa ili kuepuka
kujirudia kwa makosa yale yale. “Mwizi
aliyekuibia jana, leo hawezi kuwa mshauri wa ulinzi wa nyumba yako.
Wale walioishauri serikali kuingia kwenye mikataba mibovu ndio hao
wanashauri tena tuingine kwenye mikataba ya gesi haraka,” alisema.
Khamis Kingwangala (CCM) naye apinga mikataba bila sera
Mbunge
wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala (CCM) alitaka sera, sheria na kanuni za
gasi asilia viwepo kwanza ndipo mikataba ifungwe ili kuepusha migogoro.
Wabunge hawakuunga mkono mikataba bila sera
Wabunge
wengine waliopata fursa ya kuchangia nao waliunga mkono wenzao wakisema
kuwa rasilimali zinazopatikana eneo lolote nchini ni za Watanzania wote
na hivyo kupendekeza wananchi wapewe elimu ya kutosha pamoja kuwekewa
mazingira ya kunufaika na uwekezaji. Walipendekeza kuwa sera inapaswa
kuwawezesha Watanzania kuwa na hisa kwenge gesi hiyo, lakini wakataka
ioneshe muda maalumu wa kukamamilika wa sera, sheria na kanuni.
Waziri Sospeter Muhongo ajitetea ugawaji vitalu kiholela
Mapema
akifungua semina hiyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alisema kuwa wale wanaopotosha kuwa wizara imegawa vitalu wana
ajenda yao ya siri ya kuikwamisha nchi kiuchumi. Alifafanua kuwa
kilichofanyika ni kutangaza vitalu hivyo ili wawekezaji waombe na kwamba
Oktoba 25 mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete atafungua rasmi mpango huo wa
kujitangaza. “Mei 9, 2014 tunafungua hizo tenda kwa wale waliochukua
nyaraka zetu na kesho yake tarehe 10 ndipo tunaanza kuvigawa hivyo
vitalu. Wakati huo sera na sheria mpya ya gesi itakuwa imeshapitishwa na
kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili,” alisema. Alisema kuwa uchumi ni
umeme na kwamba hakuna njia ya mkato, lazima kuzalisha umeme wa gesi
wapende ama wasipende.