KWA UFUPI Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwarwanda alisema watuhumiwa hao
walikuwa wakisakwa kwa muda mrefu kutokana na mtandao mkubwa waliokuwa
nao, hatimaye baadhi wamefanikiwa kukamatwa huku wengine bado
wakiendelea kutafutwa.
Sumbawanga.
Polisi katika Mkoa wa Rukwa likishirikiana na Polisi wa Tabora pamoja
na kikosi kazi maalumu cha kitaifa, limefanikiwa kuwatia nguvuni watu
tisa waliokuwa wakisakwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za kumkata mkono,
Mwigulu Matonange(10) mlemavu wa ngozi Februari 15 mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwarwanda alisema watuhumiwa hao
walikuwa wakisakwa kwa muda mrefu kutokana na mtandao mkubwa waliokuwa
nao, hatimaye baadhi wamefanikiwa kukamatwa huku wengine bado
wakiendelea kutafutwa.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Weda Mashilimu(29),Nickon Kadogoo(25),
Peter Msabato(32),Ignas Sungura(27),Faraja Mwezimpya (31) pamoja na
Kurwa Hamis (29) wote wakiwa ni wakazi wa Kijiji ha Ilemba Rukwa.
Aliwataja watuhumiwa wengine ambao ni Hamis Mnywanywa ambaye ni mganga
wa jadi na mkazi wa Karema Katavi,James Paskali(24) mkazi wa majimoto,
pamoja na Ibrahimu Tella(27) mkazi wa kijiji Masanula-Usule Shinyanga.
Kamanda alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulifuatia uchunguzi wa
kina uliokua unafanywa na polisi hao kupitia mawasiliano ya simu na
taarifa mbalimbali za kipelelezi ambapo siku ya April 22 walifanikiwa
kumnasa Nickon Kadogoo akiwa Katavi na mkono huo akiupeleka mkoani
Tabora ambapo angepata soko.
Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa huyo alidai kuwa yeye na wenzake hao
waliagizwa mkono huo na mganga wa jadi aitwaye Rashid Manywanywa, ambapo
aliwaahidi angemlipa kila mmoja Sh600 milioni kama wangempelekea mkono
huo.
Alisema baada ya tukio la kumkata mtoto huyo mkono na kumpelekea mganga
huyo alidai kuwa hana fedha zote hizo kwani wao walishindwa kutumia
akili kwa kuwa hata yeye ni maskini angelipata wapi fedha zote hizo,
hivyo hawezi kununua mkono huo.
Baada ya kuona soko limeshindikana ndipo walipoamua kufanya mawasiliano
na watu wengine na kuhakikishiwa katika Mikoa ya Tabora na Shinyanga
kuna soko la uhakika ndipo safari ya kuelekea huko ikaanza.
Kwa upande wake, mganga huyo wa jadi alikiri kuwaagiza watuhumiwa hao
mkono huo na kudai kuwa alitaka kutumia kutengenezea chombo cha usafiri
ambacho alidai kuwa ni ungo ambao unatumika na wachawi kusafiria nyakati
za usiku.