Mrakibu
wa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani Bonaventura Nsokolo
akizungumza jambo na waandishi wa habari kuhusu siku ya usalama
barabarani, kulia kwake ni Bw. Alpherio Nchimbi Afisa Mtendaji Mkuu wa
Helmet Vaccine Initiative Tanzania.(Picha na Genofeva Matemu – MAELEZO).
Afisa
Mpango Mwandamizi Bw. Peter Amos akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam kuhusu wiki ya nenda kwa usalama barabarani
itakayofanyika tarehe 11 Mei, 2013 katika shule ya Sekondari Turiani
iliyopo Kinondoni jijini Dar es salaam. (Picha na Immaculate Makilika –
MAELEZO).
Na Elphace Marwa – MAELEZO.
Shirika
lisilo la kiserikali linalojishughulisha na usalama barabarani AMEND
Organisation kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama
barabarani wameandaa matembezi mafupi ya kuukumbusha umma kuhusu hatari
za barabarani wanazokabiliana nazo watembea kwa miguu.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Afisa Mpango
Mwandamizi wa AMEND Bw. Peter Amos amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka
2012 takribani watu wasiopungua elfu nne walipoteza maisha kwa ajali
za barabarani ambapo asilimia 30 kati yao ni watembea kwa miguu.
Bw.
Amos amesema kuwa matembezi hayo yatafanyika Jumamosi tarehe 11 mwezi
Mei kuanzia saa tatu asubuhi katika shule ya Sekondari ya Turiani wilaya
ya Kinondoni.
Aidha
Amos amesema matembezi hayo yanalenga kuhamasisha watu kuchukua
tahadhari wanapokuwa barabarani ili kulinda usalama wao na watembea kwa
miguu.
Bw.Amos
ameeleza kuwa jumla ya madereva 300 wa bodaboda wamepatiwa mafunzo na
wameweza kufaulu vipimo vya udereva na kupatiwa leseni .
Kwa
upande wake Mrakibu wa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani
Bonaventura Nsokolo kutoka trafiki Makao makuu ametoa wito kwa
waandishi wa habari kuelimisha jamii juu ya matumizi bora ya barabara
kwani ajali za barabarani zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania
wengi wasio na hatia.
Wakati
huo huo Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Helmet
Vaccine Initiative Tanzania Bw. Alpherio Nchimbi amesema taasisi yake
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na wadau wengine wana lengo la
kupunguza kwa asilimia 50 vifo vinavyotokana na ajali za barabarani
kufikia mwaka 2020.
Wageni
rasmi akiwemo Kamanda Mpinga wa Kikosi cha Usalama barabarani
wanatarajiwa kuzungumza na wananchi siku hiyo ili kuwahamasisha
kujilinda na ajali za barabarani na kupunguza vifo vitokanavyo na ajali
za barabarani.



