Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amedai
kuwa amenasa taarifa za siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa
Serikali ya sasa kukaa madarakani.
Rais Jakaya Kikwete
Profesa Lipumba alisema hiyo inatokana na wasiwasi kuwa mchakato wa
Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014 hivyo kutokuwa rahisi kwa
uchaguzi kufanyika mwaka 2015.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la
CUF, Profesa Lipumba alisema kuwa Serikali inataka kuongezewa muda wa
kukaa madarakani kwa miaka miwili ikimaanisha kuwa Serikali ya Awamu ya
Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete itakaa madarakani hadi mwaka 2017.
Hata hivyo, madai hayo ya Profesa Lipumba yamepingwa vikali na Serikali
na viongozi wake watatu waandamizi ambapo walijibu walipoulizwa kwa
maandishi na mwandishi wetu mjini Dodoma wanakohudhuria kikao cha Bunge.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alijibu: “Mchakato wa Katiba
upo ‘on track’ (unakwenda vizuri) hatuna sababu ya kufanya hivyo.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijibu”“Njooni ofisini kwangu nitasema ni kitu gani.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William
Lukuvi alijibu kwa utani bila ya kufafanua: “Njooni niwajuze, unajua
kamba haitoki Ukambani kama ilivyo kamba.”
Profesa Lipumba amemwomba Rais Kikwete asilikubali wazo hilo akisema
wananchi hawatakubali na taifa linaweza kuingia katika mtafaruku.
“Nitapenda kuona Rais Kikwete akikataa jambo hilo kwani litachafua
taswira ya nchi. Hatua hii ni kinyume cha utawala bora,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema Serikali haipaswi kuhofia uchaguzi kwa sababu ya Katiba kwani
bado uwezekano wa kuandaa uchaguzi wa haki na huru unawezekana kwa
utaratibu mwingine.
“Mchakato wa Katiba unaendelea, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatuambia
kwamba mwaka 2014 tutakuwa na Katiba Mpya, sasa CUF tunasema kwamba hata
kama Katiba Mpya haitapatikana kwa kipindi hicho kuwe na Tume huru ya
Uchaguzi,” alisema Profesa Lipumba.
Jukwaa la Katiba kutinga mahakamani
Siku nne baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu ya mwongozo
kuhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba, Jukwaa la Katiba Tanzania
(Jukata), limesema litafungua kesi mahakamani kutaka kusitishwa kwa
mchakato mzima wa Katiba Mpya kwa madai kuwa uendeshwaji wake umejaa
mizengwe, itikadi za vyama na rushwa. Limetaja sababu tano ambazo
zimekiukwa.
Limesema kesi hiyo itasimamiwa na timu ya mawakili 10 watakaoongozwa na
Mwanasheria wa masuala ya Haki za Binadamu, Dk Rugemeleza Nshala na
itawasilishwa mahakamani siku saba zijazo kuanzia jana.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Jukata, Deus Kibamba alitaja sababu hizo kuwa ni kutokufanyiwa
marekebisho katika sehemu tatu za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kama
ilivyoahidiwa na Rais Kikwete, kuvurugwa kwa Uchaguzi wa Mabaraza ya
Katiba, mchakato wa Katiba kukosa uongozi, kuminywa kwa demokrasia
wakati wa mchakato huo pamoja na Jukwaa hilo kuzuiwa kuonana na Rais ili
kueleza upungufu uliopo.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi