Mtuhumiwa Simon Jumbe anayetajwa kujifanya afisa wa Takukuru.TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kumnasa mtu mmoja ambaye anasadikika kuwa mkuu wa genge la watu wanaojifanya Maafisa wa Ofisi ya TAKUKURU Mkoani hapa.Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari ofisini kwake Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Ayubu Akida alisema kwamba kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Simon Jumbe (32) lakini amekuwa akitumia majina mengie kwa kujiita Mapunda na SP ni kutokana na mtego uliowekwa na maafisa wake. |
Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza Ayoub Akida, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo. |
“Tuliweka
mtego huo kutokana na kuwepo taarifa za siri kutoka kwa raia wema
ambapo walitueleza kwamba kuna wimbi la baadhi ya watu ambao wamekuwa
wakiwadanganya watu kuwa wao ni maafisa na watumishi wa TAKUKURU baada
ya kuweka mtego Mei 13 mwaka huu tumefanikiwa kumnasa huyu maeneo ya
Kata ya Mkuyuni Wilayani Nyamagana” alisema Akida.
Kamanda
Akida alieleza kwamba tangu mwezi April na Mei tumekuwa katika hekaheka
za kuwatafuta watu hao baada ya taarifa za kuwepo watu hao
wanaojitambulisha kuwa watumishi na wamekuwa akiwadanganya watu na
kufanya kazi ambazo si za ofisi ya Takukuru ikiwa ni zile za Taasisi
zingine za serikali.
Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza Ayoub Akida |
“Katika
kipindi hicho tuliweza kupokea taarifa za matukio kumi ya kutoka kwa
watu waliotapeliwa katika Wilaya za Misungwi na Jiji la Mwanza ambapo
baada ya kumnasa mtuhumiwa huyu na kumhoji alidai kuwa yeye peke kwa
kutumia utapeli huo ameweza kujipatia kiasi cha shilingi milioni
4,637,000/= kutoka kwa watu kumi na mbili”alisema Kamanda.
Naye
mmoja wa watu walioathirika na kutapeliwa aliyejitambulisha kwa jina la
James Belindo mkazi wa Nyakato Buzuruga Wilayani Ilemela alisema kwamba
alimfahamu mtuhumiwa kwasababu alikuwa jirani yake naye mtuhumiwa
alitumia mwanya huo wa ujirani akimweleza kuwa kuna magari 12 yameletwa
ofisini kwao yaani Takukuru hivyo kuna nafasi za kazi ambazo anaweza
kumuunganishia.
James Belindo mmoja kati ya waliotapeliwa. |
“Alidai
kama nina ujuzi wa kuendesha gari yaani udereva basi nimwambie,
nilimweleza sina lakini kuna jamaa yangu, naye akasema hamna tabu
nimpeleke atakuwepo ofisi ya Takukuru Mkoa, akaomba vyeti na leseni
kisha akamweleza kuwa inatakiwa kufunguliwa majarada matano na kuomba
kiasi cha 475,000/- lakini hakupata kazi hiyo”alieleza kwa masikitiko.
Kamanda
Akida amewatahadharisha wananchi kuwa makini na kundi la matapeli hao
wanaojifanya watumishi wa Takukuru ambao wamekuwa wakiidhalilisha na
kuipaka matope ofisi yake na kuharibu taswira iliyopo kwa jamii na
kuwataka kufika ofisi za Takukuru na kutotoa fedha bila utaratibu wa
taasisi hiyo.
Aidha
alisema kwamba kutokana na kuwepo kundi hilo ofisi yake imewataka
wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri zitakazofanikisha kunaswa kwa
watu hao ambao wamekuwa wakiwadanganya kuwatafutia kazi,kuwatisha ili
wawapatie fedha kunyume na huduma zinazotolewa na ofisi za Takukuru
Wilayani na Mkoa.