Maskini! Mama mzazi wa aliyekuwa msanii maarufu wa vichekesho na muziki Bongo, Marehemu Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kufunga safari kutoka Tanga hadi Dar kwa ajili ya kushughulikia fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya mwanaye na kuambulia patupu.
“Namshukuru Mungu kwa yote maana nimerudi Tanga kama nilivyotoka na nauli yangu kwani sikukuta fedha yoyote kwenye akaunti zote za Sharo ila inawezekana alichukua fedha zote kwa ajili ya manunuzi yake kabla ya kifo.
“Huwezi jua kwani alikufa kwa ajali hivyo ni lazima vitu vyake vingi vibaki gizani,” alisema mama Sharo na kuongeza:
“Sioni haja ya kumlaumu mtu zaidi ya kumuachia Mungu ambaye ndiye muweza wa yote, hapa duniani sote tunapita.”
Sharo Milionea alipatwa na umauti Novemba mwaka jana kwa ajali ya gari katika eneo la Songa- Maguzoni wilaya ya Muheza mkoani Tanga wakati akiwa safarini akitokea Dar es Salaam kuelekea nyumbani kwao, Kijiji cha Lusanga, Muheza mkoani Tanga.