Ripoti kutoka Syria zinasema
kuwa wanajeshi wa serikali wamefanya shambulio la kuuteka tena mji wa
Qusayr unaodhibitiwa na wapiganaji, baada ya mapigano ya majuma kadha
katika eneo linalozunguka mji huo.
Wanaharakati wanasema mashambulio makubwa ya mizinga yameuwa watu 20.
Mji wa Qusayr ni muhimu kwa wapiganaji na uko katikati baina ya Damascus na bahari ya Mediterranean.
Huku nyuma Rais wa Syria, Bashar al-Assad, ameionya Marekani kwamba juhudi zake za kutaka mazungumzo ya amani yafanyike hazitazuwia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Akihojiwa na gazeti moja la Argentina, Clarin, Bwana Assad alikariri kuwa hana azma ya kuondoka madarakani mpaka mwaka wa 2014 ambapo uchaguzi wa rais unatarajiwa kufanywa.
Marekani na Urusi zinajaribu kuandaa mkutano mjini Geneva mwezi ujao ili kutafuta amani.
Mkutano unatarajiwa kujumuisha maafisa wa serikali ya Bwana Assad na wapiganaji wanaojaribu kumuondoa madarakani, lakini rais wa Syria alisema upinzani umegawika mno kuweza kuzungumza makubaliano.