Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Wednesday, May 15, 2013

JAJI WARIOBA: JUKWAA LA KATIBA RUKSA KWENDA MAHAKAMANI

 


Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema haimzuii mwananchi, asasi au taasisi yoyote kufungua kesi
Mahakamani kupinga au kuzuia mchakato unaoendelea wa Katiba Mpya.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi huo kwa baadhi ya waandishi wa habari
waliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Mei 15, 2013) kutaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyotolewa na Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam jana (Jumanne, Mei 14, 2013).
Katika tamko lake, Jukwaa la Katiba lilieleza nia ya asasi yake kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania
ndani ya siku saba ili kusimamisha mchakato wa katiba Mpya kutokana kile ilichodai ni kasoro zinazojitokeza katika mchakato wa katiba unaoendelea.
Ruksa kwenda Mahakamani
Hata hivyo, akiongea na baadhi ya waandishi wa habari waliofika leo ofisini kwake leo, Jaji Warioba
alisema Tume yake haina tatizo na mtu au asasi kwenda Mahakamani kwa kuwa hiyo
ni haki yao ya kikatiba.
“Nimesoma tamko lao na niseme tu halina jipya. Hii si mara ya kwanza kusikia hili (la kwenda
Mahakamani), na jibu letu lilikuwa waende na ndio jibu letu hadi sasa,”
alisema
Jaji Warioba anayeongoza Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 2 mwaka jana.
“Mimi nasema waende ili tujue Jukwaa haswa ni nani, kwa sababu ninafahamu ni mkusanyiko wa asasi mbalimbali na baadhi ya asasi hizohizo zimetuletea maombi ya kuunda Mabaraza ya Katiba ya
Taasisi na Asasi… sasa jukwaa hili ni nani haswa?,” alisema Jaji Warioba.
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
Kuhusu marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba amesema kuwa ingawa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sio jukumu la Tume, wanafahamu kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kurekebisha sheria hiyo kama ilivyoahidiwa.
“Hili la marekebisho ya sheria ingawa sio jukumu letu, lakini nalo sio jipya. Wote tulimsikia Waziri
Mkuu hivi karibuni kule Bungeni akisema kuwa Serikali inaandaa marekebisho ya Sheria hiyo yatakayowasilishwa Bungeni … sasa hawa wanataka nini?,” alihoji Jaji Warioba.
Tume ina watu wenye weledi na uadilifu mkubwa Kuhusu, mchakato wa Katiba
kukosa uongozi madhubuti, Mwenyekiti huyo amesema kuwa Tume yake imeundwa na
watu wenye sifa, weledi na uadilifu mkubwa ambao wametokana na mapendekezo ya wadau
mbalimbali yakiwemo makundi, vyama, asasi mbalimbali za kijamii na kiraia.
“Mimi najivunia kuongoza Tume yenye watu wenye weledi na uadilifu mkubwa na wananchi wanalifahamu hili na kwa kweli wanatuunga mkono,” alifafanua Jaji Warioba. 
Muda wa kutolewa Rasimu ya Katiba
Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba pia alifafanua kuhusu muda ambao Tume yake inatarajia kutoa Rasimu ya Katiba kwa lengo la kujadiliwa na kutolewa maoni katika Mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba,
hivi sasa Tume inaendelea kuandaa Rasimu ya Katiba na wananchi watapata muda wa
kutosha kuijadili na kutoa maoni yao.
“Mpango wa Tume ni kukamilisha kazi zake ndani ya muda uliopangwa na sheria... tutatoa Rasimu ya
Katiba katika muda ambao utatosha kuwafanya wananchi na wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba kuisoma,” alifafanua Jaji Warioba.
Jaji Warioba pia ameelezea kushangazwa kwake na kauli za wadau mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Tume na kusisitiza kuwa wananchi na wadau wengine wasubiri Rasimu ya Katiba itolewe na
Tume ndipo watoe maoni.
“Nadhani itakua ‘fair’ (sawa), tukishatoa rasimu ndiyo watu watuhukumu,” alifafanua Mwenyekiti huyo
ambaye pia alishawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Tusiwabeze Wananchi
Kuhusu madai kuwa wananchi waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya hawana uwezo na waledi wa kujadili na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba, Jaji Warioba amesema
madai hayo hayana msingi na yanabeza maamuzi ya wananchi.
Mwenyekiti huyu ameongeza kuwa uamuzi wa Tume kushirikisha wananchi kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji,
vitongoji na shehia ulilenga kuwapa wananchi hao fursa ya kuchaguana na
kuongeza kuwa wananchi walitumia fursa hiyo vizuri.
“Wanaosema haya wanawabeza wananchi waliowachagua hao wajumbe,” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake imezipata zinaonyesha kuwa katika wajumbe hao kuna
wananchi wasomi na wenye weledi wa kutosha kujadili rasimu ya katiba.
Mwisho.
Omega S. Ngole,
Principal Information Officer,
Constitutional Review Commission (Tanzania),
Ohio Street, 
PO Box 1681,
Dar es Salaam,
Tel: +255 (0) 22 2133425,
Fax: +255 (0) 22 2133442,
Mobile: +255 (00 757 500800,
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...