"Sifahamu iwapo Kerry ama yeyote mwingine amepata madaraka ya watu wa Syria kuzungumzia kwa niaba yao juu ya nani anapaswa kuondoka madarakani na nani anapaswa kubaki. Suala hilo litaamuliwa na watu wa Syria katika uchaguzi wa rais mwaka 2014.
Mkutano wa upatanishi
Hata hivyo amesema kuwa anakaribisha juhudi za Marekani na Urusi za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilivyodumu kwa muda wa miaka miwili sasa.
"Tumepokea hatua ya Urusi na Marekani kwa vizuri na tuna matumaini kuwa kutakuwa na mkutano wa kimataifa kuwasaidia Wasyria kumaliza mzozo wao." Gazeti la Clarin limemnukuu Assad akisema.
Ameongeza hata hivyo kuwa, " Hatuamini kuwa mataifa mengi ya magharibi yanataka kweli suluhisho nchini Syria. Na hatufikiri kuwa mataifa yanayowasaidia magaidi yanataka suluhisho katika mzozo huu."
Magaidi nchini Syria
Syria inawaita waasi ambao wamekuwa wakipigana kuuondoa utawala huo kuwa ni " magaidi".
Jana Jumamosi (18.05.2013) televisheni ya taifa imewashutumu wale iliyowaita magaidi kwa kuripua bomu lililokuwa limetegwa katika gari katika kitongoji cha kaskazini mwa mji mkuu Damascus , ikisema kuwa kiasi watu watatu wameuwawa na wengine kadha wamejeruhiwa.
Shirika hilo la televisheni la taifa limesema bomu hilo liliwekwa katika gari katika kitongoji cha Rokn Eddin na kwamba kikosi cha kutegua mabomu kilipelekwa katika eneo hilo kutegua bomu jingine.
Shambulio la bomu
Televisheni ya taifa imesema kuwa shambulio hilo la bomu lilitokea katika sehemu ya kuegesha magari karibu na shule na msikiti.
Shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu mjini London pia limeripoti kuhusu shambulio hilo la bomu, lakini limetoa idadi ya juu ya watu waliofariki kuwa ni wanane na wengine 10 wamejeruhiwa.
Taarifa imesema kuwa shambulio hilo la bomu lililenga magari ya jeshi la serikali, na kuuwa wanajeshi wanne wa kawaida na raia wanne.
Hakuna kundi lililodai mara moja kuhusika na shambulio hilo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Sudi Mnette