![]() |
| Askari wakiwa lindoni/doriani, Mtwara |
Hali
ya usalama katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa imezidi kuwa
mbaya baada ya askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka
wanawake na kumpiga risasi mjamzito
Mbali
na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi
katika mtaa wa Magomeni na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu
vilivyomo ndani.
Hata
hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa anasema hali
ni shwari na kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao kama
kawaida.
Kaimu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi
amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni,
zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti
zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18:
“Ni
kweli kwa leo( jana) tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni
mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni.pia tumepokea mwanafunzi
wa shule ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.”
Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake.
Huduma
za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyo wazi, hakuna usafiri wa
daladala wala pikipiki, mji upo kimya, sauti za milio ya mabomu na
bunduki zimetawala, wanajeshi waliovalia sare wameuzingira mji wakiwa
katika magari na pikipiki.
Wakizungumza
na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti wakazi hao wamelalamikia
kitendo cha askari wa jeshi la polisi kuingia katika makazi yao,
kuwapiga, kuwabaka na kuwapora mali zao:
“Magomeni
A hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga na
kutunyang’anya simu, yani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepoteza
watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi” alisema Paulina Idd na
kuongeza:
“Majumba
yetu yamechomwa moto , wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu
wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu halafu tunateseka sisi yaani
tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” alisema Paulina.
![]() |
| Wanawake na watoto wakiwa hospitali ya rufaa ya Ligula, Mtwara kwa ajili ya kuomba hifadhi baada ya kuyakimbia makazi yao kwa hofu |
Kamanda
Sinzumwa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa atapingana na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Emmanuel Mchimbi aliyewasili Mtwara leo: “Kuhusiana na suala
hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani nitapingana na Waziri wangu
kwani leo ametoa tamko bungeni na leo atawasili,” alieleza Sinzumwa
Wananchi wazungumzia bajeti
Wakizungumzia
uwasilishwaji wa hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini wakazi wa hapa
wamesema kuwa hawakubaliani na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwani
mpango huo utawaletea dhuluma:
“Mpango
wa kusafirishwa kwa gesi asilia hatuna mpango nao kwa wakazi wote wa
Mtwara kwa kifupi akina mama wa mtwara hatutaki itoke,” alisema Fatuma
Abdallah.





