Baadhi ya wajumbe wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo, wakizungumza na waandishi. |
Katibu wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo, Badi Darusi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam |
Katibu wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo, Badi Darusi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo |
Mkutano na wanahabari leo |
Na Mwandishi Wetu
WASHIRIKI
wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo (GDSS)
linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wamejitokea na
kulalamikia mchakato mzima wa upatikanaji wajumbe wa mabaraza ya Katiba
uliofanyika maeneo mbalimbali hivi karibuni. Wawakilishi hao ambao
baadhi yao walishiriki kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi, wametoa
malalamiko hayo leo jijini Dar es Salaam walipokuwa wakizungumza na
vyombo anuai vya habari.
Akizungumza
katika mkutano huo na wanahabari, Katibu wa jukwaa hilo, Badi Darusi
kutoka TOWSF, alisema kulikuwa na dosari nyingi katika uchaguzi wa
wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya uliofanyika hivi karibuni, hivyo
kuitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba ifanye tathmini ya zoezi zima na
kuangalia namna ya kuondoa kasoro hizo.
Alisema
kwa baadhi ya maeneo baadhi ya wasimamizi wa mchakato huo ngazi za
mitaa waliingiza itikadi za vyama, dini na pia kuwepo kwa mazingira ya
rushwa hivyo kushauri kuna kila sababu ya mchakato huo kwa mkoa wa Dar
es Salaam urudiwe upya ili haki itendeke.
Alisema
vyama vya siasa vilikuwa vinatumia fursa ya kufanya kampeni chafu
kinyume na utaratibu na muongozo uliowekwa na Tume ya Taifa ya
mabadiliko ya Katiba, na kuongeza kuwa katika baadhi ya mitaa waliongeza
sifa ya kuwa mwanachama wa chama fulani ili uchaguliwe kuwa mjumbe wa
baraza la katiba jambo ambalo ni kinyume na maelekezo yaliyotolewa na
tume.
“Tumeshtushwa
sana na namna mchakato huu ulivyogubikwa na kasoro mbalimbali ambazo
zisipochukuliwa hatua madhubuti tunaweza tukawa na katiba ambayo
haitokani na wananchi. Mchakato huu uligubikwa na vitendo vya udini,
siasa, rushwa, vitisho na ubaguzi wa kijinsia. Hali hii ilipelekea
baadhi ya watu waliokuwa na sifa za kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba
kuenguliwa kimakosa kutokana na utashi na maslahi binafsi ya watu
wachache,” alisema Darusi.
Aidha
alitolea mfano katika mitaa ya Msakuzi, Kata ya Mbezi na Mtaa wa
Mbagala Rangitatu kata ya Charambe wagombea wa ujumbe wa mabaraza ya
katiba ambao hawajulikani misimamo yao katika siasa waliulizwa wazi wazi
kuwa wao ni wafuasi wa chama gani na baadhi ya viongozi wa mitaa ambao
ndio walikuwa wasimamizi wakuu wa mchakato huo.
“Mfano
hai ni kata ya Mabibo yenye wakazi 72,000 (sensa ya 2002) imeshindwa
kupata wajumbe wa mabaraza ya katiba kwa sababu ya wajumbe 7 wa baraza
la maendeleo la kata (WDC) kushindwa kuafikiana eti kila mmoja akitaka
mtu wa chama chake ndio awe mjumbe wa baraza la katiba la wilaya ya
kinondoni kinyume na maelekezo na muongozo wa kuwapata wajumbe hao
uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hali hii inawafanya wakazi
wa kata ya mabibo kukosa uwakilishi katika baraza la katiba la wilaya,”
alisema kiongozi huyo.
Aliongeza
kuwa mchakato huo pia uligubikwa na vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji
wa jinsia uliofanya na baadhi ya viongozi wa mitaa na vyama vya siasa,
kwenye baadhi ya mitaa wasichana waliokuwa na umri wa miaka 18 hadi 35
walienguliwa katika kundi la vijana na kuwekwa katika kundi la Wanawake
watu wazima kinyume na utashi wa mtu binafsi aliyegombea. Mfano ni mtaa
wa Mbagala Rangi Tatu kata ya Charambe.
Hata
hivyo waliiomba Serikali na Tume ya Mabadiliko ya Katiba zichukue hatua
madhubuti za kukabiliana na vitendo vya udini vinavyoshika hatamu kwa
mgongo wa mchakato wa katiba mpya ili kuhakikisha katiba haiundwi kwa
itikadi za mazingira hayo.
Alisema
endapo mchakato huo utarudiwa walipendekeza Kamati ya Maendeleo ya Kata
isiwe na dhamana ya kuwachagulia wananchi wajumbe wa mabaraza ya katiba
kwani wengi wanaongozwa na utashi wa kisiasa na wananchi pekee ndio
wawe na dhamana ya kuwachagua wawakilishi wao.
”Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iangalie namna mpya ya kuyashirikisha makundi
ya watu walio pembezoni kwenye mabaraza ya katiba ili kuwa na uwakilishi
katika kujadili rasimu ya katiba. Mfano muongozo uliotolewa na tume
hauja ainisha ni namna gani watu wenye ulemavu watashikiriki katika
kuingia kwenye mabaraza ya katiba ya wilaya,”
Mchakato
wa katiba mpya usiendeshwe kwa haraka kwani unawafanya wananchi walio
wengi wasiwe na taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea katika mchakato
huu wa uundaji wa katiba mpya. Tume ya katiba iangalie mfumo wa
kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu mwenendo wa mchakato wa katiba mpya
nchini kwani taarifa nyingi hazifiki kwa wananchi walio wengi na kwa
wakati.