Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Monday, June 3, 2013

NAPE;MPANGO WA SIRI WA MAUAJI WA CHADEMA WAGUNDULIKA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akihutubia katika moja ya mkutano mkoani Njombe.
Na Mwandishi Wetu Makambako


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeibua mipango ya siri ya mauji inayoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa kuwahusisha askari Polisi na wananchi wa kawaida.
Hatua hiyo ya CCM kuvunja ukimya kuhusu sakata hilo liliibuliwa jana mjini hapa na Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi wa Makambako na vitingoji vyake.
Katika mkutano huo Nape, alisema kuwa kumekuwa na mipango inayoratibiwa na CHADEMA ya kufanya maandamano ambayo yataambatana na mauji dhidi ya askari Polisi na wananchi wa mji huo.
Alisema mipango hiyo imekuwa ikiratibiwa kwa mwezi mmoja sasa kwa kufanyika vikao katika maeneo tofauti kwa kuwahusisha viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho cha upinzani.
“Ninapenda kuweka wazi jambo moja kwa mujibu wa taarifa za siri ambazo CCM imezinasa kutoka ndani ya CHADEMA ni kwamba hivi sasa chama hiki kipo katika mikakati ya kufanya maandamano katika miji minne ikiwemo Makambako.
“Lengo la maandamano hayo ni kuibua vurugu zitakazosababisha mauji dhidi ya askari Polisi na raia wa kawaida ili kutafuta umaarufu wao ambao umeanza kupungua kwa siku za hivi karibuni.
“CCM inapenda kuwaambia Watanzania popote pale walipo wajue kuwa CHADEMA si chama cha siasa, bali ni genge la watu ambalo limejikusanya kwa lengo la kuua na kung’oa kucha watu. CCM haiko tayari kuona nchi inaingia katika shimo la mauji ya kupanga hata kidogo.
“Kwa wiki moja sasa wamekuwa wakichagua miji ya kufanya maandamano yao ambayo yataambana na mauaji na wamepanga kufanya katika miji ya Makambako, Songea pamoja na miji ya Ilula wilayani Kilolo pamoja na mji wa Ruaha wilayani Kilombero,” alisema Nape huku akishangiliwa na umati wa wananchi katika mkutano huo.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, alisema kwa muda mrefu chama chake kimekuwa kimya na kuacha vyombo vya dola vifanye kazi yake hasa kwa watu ambao wamekuwa wakitaka kulitumbukiza taifa katika machafuko kwa kivuli cha siasa.
Alisema kutokana na hali hiyo hivi sasa CCM haitakuwa tayari kuona mauji kutokea tena nchini kama ilivyokuwa katika miji ya Arusha, Morogoro na Iringa.
“Ni wazi siku tatu kabla ya maandamano ya Morogoro yaliyosababishwa kifo cha kijana mmachinga asiye na hatia, CCM ilijitokeza mbele ya umma wa Watanzania na kuwaambia kuwa kuna mipango ya mauaji inayopangwa na CHADEMA kwa kutoa watu jijini Dar es Salaam.
“Ilipotimu siku hiyo walifanya hivyo kwa kutoa magari kila kona ya jiji la Dar es Salaam na kwenda kuwaingia vijana maskini wa Morogoro katika maandamano ambayo yalipigwa marufuku na Polisi.
“Haikupita muda alikufa kijana wa kitanzania bila hatia huku Mbowe na babu Slaa wakiwa Dar es Salaam wakiendelea na kazi zao huku wakifanya mashauri na familia zao. Kama wao kweli wana uchungu na nchi hii kwani hatuwaoni wakiwa mbele ya maandamano,” alisema Nape.
Kutokana na kauli hiyo Nape, alisema kuwa moja ya kazi anayoifanya Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, ni kwenda mjini Songea ambapo atafanya kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi na kumueleza mipango hiyo michafu inayolenga kuharibu sifa ya Tanzania.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...